DC Geita aonya utitiri wa mikopo ya pikipiki halmashauri

MKUU wa Wilaya ya Geita, Hashimu Komba amezitaka halmashauri kubuni miradi mbadala kwa ajili ya kukopesha vikundi maalum badala ya kujikita zaidi katika kukopesha pikipiki (bodaboda) na bajaji.
Komba ametoa kauli hiyo katika hafla ya halmashauri ya wilaya ya Geita kukabidhi mkopo wenye thamani ya Sh bilioni 1.15 kwa vikundi 111 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kauli yake inakuja baada ya halmashauri kuambatanisha jumla ya pikipiki 43 na bajaji tano kama sehemu ya mkopo huo ikiwa ni njia ya kuwapa vitega uchumi walengwa waliokidhi vigezo.
“Wasiwasi wangu itakuja kufika hatua bodaboda zitakuwa nyingi kuliko abiria.Sasa tutaanza kupangiana zamu, nani aingie, nani asiingie kwenye egesho”, amesema na kuongeza;
“Mimi niwaambie fedha zipo za kutosha, tunataka vikundi vyetu vikue. Hatujazaliwa kuishia kwenye bodaboda, hatujazaliwa kuishia kwenye bajaji, ni lazima tukue”.
Komba ameitaka halmashauri kuendelea kuvijengea uwezo na kuviongezea mitaji vikundi vilivyoonyesha matokeo chanya wa uzalishaji na ubunifu katika miradi ili waweze kufikia uwekezaji mkubwa zaidi.
Ameagiza maofisa maendeleo kutiilia maanani maandiko mradi ya waombaji wa mikopo na kuyapitia kwa kina ili kuwashauri na kisha kutoa fedha iwapo malengo yao yatakuwa yana tija.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Karia Rajab amewataka wanufaika kusimamia kwa umakini dhamira yao na kufanya kazi kwa bidii ili waweze kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Awali Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri, Jonas Kilave, amebainisha kuwa jumla ya vikundi 155 viliomba mikopo, lakini vikundi 111 pekee ndiyo vilivyokidhi vigezo vya kupata mkopo.
Aidha taarifa kutoka ofisi ya maendeleo ya jamii ya halmashauri ya wilaya ya Geita inaonyesha kuwa tangu Januari hadi Julai 2025 halmashauri imetoa mkopo wa pikipiki 98, bajaji tano za abiria na bajaji mbili za mizigo.



