SONGWE; MKUU wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi amewaasa wananchi wa Wilaya ya Ileje kuungana, na kushirikiana kwa pamoja kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Amewataka pia kukemea na kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, ili kuhakikisha jamii inabaki salama dhidi ya vitendo hivyo.
Akizungumza leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia wilayani hapa, alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, Mgomi alitoa wito kwa wananchi kubadilika na kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Amesema vitendo hivyo vinarudisha nyuma ustawi wa jamii na kuzorotesha uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Amewasihi wazazi kuwalinda watoto kwa kuwapa malezi stahiki yanayozingatia maadili ya Kitanzania, ili kuwaepusha watoto kuiga tamaduni za nje, ambazo zinakiuka miiko ya maadili ya nchi.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya aliziasa familia kudumisha upendo na kuepuka migogoro na kutumia fursa zilizopo katika wilaya, ili kujiongezea kipato kitakachowasaidia kutunza na kulea familia.