DC Kahama ajivunia matunda ya kodi wilayani kwake

SHINYANGA; MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mboni Mhita amewataka wananchi kuendelea kulipo kodi na kujivunia maendeleo mbalimbali yanayopatikana kutokana na kodi wanazolipa.
Mboni ameyasema hayo Machi 18, 2025 alipokutana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), waliofika ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha wakati wa shughuli ya utoaji elimu ya kodi ya mlango kwa mlango inayoendelea wilayani hapo.
Amesema ndani ya wilaya kuna miradi mbalimbali ambayo inatokana na kodi wanazolipa
“Kodi ambazo tunalipa ndio ambazo zinatumika na serikali kwenda kufanya maandaleo haya katika jamii… sisi wa Kahama tunajivunia hospitali ya kisasa ambayo utadhani ni ya kanda, ukiangalia zahanati za kisasa katika wilaya yetu,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa mkuu Msimamizi wa kodi kutoka TRA ambaye ni kiongozi wa timu hiyo, Lameck Ndinda ameeleza kuwa lengo la kutoa elimu ya kodi ni kusikiliza changamoto na maoni ya wafanyabiashara ili kuweza kuboresha huduma zao
Amefafanua kuwa katika utoaji huo wa elimu wamebaini kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara bado hawajakadiriwa na na wengine kutokutoa risiti vizuri, hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara kwenda kukadiriwa kabla ya tarehe 31 Machi ili kuepuka adhabu.

” Wito wangu kwa wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kwenda kukadiriwa kabla ya tarehe 31 mwezi Machi, na wakisha kukadiriwa wawahi kufanya malipo ya awamu ya kwanza,” amesema.



