DC Nyamwese: Bodaboda changamkieni fursa za mikopo

TANGA: MKUU wa Wilaya ya Handeni Salum Nyamwese, amewataka waendesha bodaboda na bajaji kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Mji Handeni kupitia mapato ya ndani ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na mikataba kandamizi.
Akizungumza katika mkutano na maofisa hao wa usafirishaji uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Chanika, mjini humo, Nyamwese amesema changamoto kubwa inayowakabili waendesha bodaboda na bajaji ni mikataba ya kinyonyaji kutoka kwa wamiliki wa vyombo vyao vya usafiri, jambo linalowarudisha nyuma kimaendeleo.
“Ni muhimu kuunda vikundi ili kupata mikopo ya halmashauri ambayo haina riba na itawawezesha kumiliki vyombo vya usafiri. Dhamira ya Rais wetu, Dk Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata maendeleo, hivyo mnapaswa kuchangamkia fursa zilizopo,” amesema Nyamwese.
Aidha, amewataka kujiepusha na vitendo vya uhalifu na kufuata sheria za usalama barabarani, huku akimkemea tabia ya baadhi ya waendesha bodaboda kufanya vitendo vya kihatarishi barabarani maarufu kama vishwandu.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Serikali ya Wilaya imeandaa mpango wa mafunzo ya bure kwa wiki moja kupitia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Handeni (FDC), yatakayowawezesha kupata vyeti vitakavyotumika katika kupata leseni za udereva.
Awali, akisoma risala ya Umoja wa Bodaboda Handeni wenye wanachama 1,265, Hamis Kidunda, ameomba serikali kuendelea kuwawezesha kupata mikopo ya pikipiki na bajaji ili kuondokana na mikopo kandamizi.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya kutuwezesha kufanya shughuli zetu kwa usalama. Pia tumekuwa tukishirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya uhalifu unaotumia bodaboda,” amesema Kidunda.



