DED Kalambo atuhumiwa ubadhilifu, matumizi mabaya ya madaraka

RUKWA: MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa wametoa tamko rasmi la kutokuwa na imani na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Shafi Mpenda wakimtuhumu kwa ubadilifu na matumizi mabaya ya ofisi.
Akisoma tamko hilo katika kikao cha dharura kilichohudhuliwa na madiwani 20 kati ya 23 ,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hilo, Bosco Kapufi alisema wanazitaka mamlaka husika zifanye uchunguzi wa kina wa matumizi na mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
“Mkurungenzi anatumia pesa mbichi zinazokusanywa badala ya kuziweka benki hatuko tayari kuendelea kufanya kazi naye. Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan atuletee Mkurungenzi Mtendaji mwingine ili kuinusuru halmashauri yetu,” amesema.
Ameongeza kuwa hofu kubwa ni halmashauri yao kufa kutokana na makusanyo ya ndani ya halmashauri hiyo kupungua kwa kasi licha ya kuwepo kwa vyanzo vya kutosha vya mapato.

Madiwani Fortunatus Zozimo wa Kata ya Msanzi,Peter Mbita wa Kata ya Kasanga na Grace Namsanda Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Mambwe Kenya wakiunga mkono tamko hilo walisema Mkurugenzi Shafi anawadhalilisha kwa kukaidi kutekeleza maagizo anayopewa katika vikao vya Baraza la Madiwani.
SOMA ZAIDI: Madiwani wampongeza Samia utekelezaji miradi
Waliongeza kuwa utekelezaji wa mradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.0 imesimama licha ya Rais Samia kuitengea fedha.
Akizungumzia sakata hili Mkuu wa Wilaya ya Kalambo,Dk Lazaro Komba amekiri kuufahamu mvutano na tofauti zilizopo baina ya madiwani wa halmashauri hiyo inayoongozwa na mwenyekiti, Daudi Sichone na Mkurugenzi Mtendaji Mpenda ambayo wamekuwa na mvutano mkubwa na kutoelewana katika vikao vya baraza la madiwani.

Aliongeza kuwa madiwani hao wameomba kukutana na Mkuu wa Mkoa ambaye ni msimamizi wa Serikali za Mitaa mkoani humo huku msimamo wao ni kutoendelea kufanya kazi na Mkurugenzi Mtendaji Mpenda.
” Wiki mbili zilizopita nimeunda timu mbili moja ikiongozwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya kuchunguza tuhuma kuwa kiasi cha Sh milioni 200 mapato yaliyokusanywa na watendaji zilitumika zikiwa mbichi bila kuwekwa Benki ; timu ya pili itafuatilia kila chanzo cha mapato ili kubaini dosari zilizopo” alieleza Dk Komba.
Aliwataka madiwani na wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki jitihada za kutatua changamoto hiyo zikifanyika bila kuathiri utendaji wa halmashauri hiyo.
Jitihada za kumpatia Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Mpenda ziligonga mwamba baada ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Halmashauri hiyo,Baraka Lusajo kueleza kuwa Mpenda amemwachia maelekezo kuwa ameenda kupumzika na hayupo tayari kukutana na waandishi kwa kuwa tuhuma hizo zimemchanganya kwa hajihisi vizuri. ”
Aliwataka madiwani na wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki jitihada za kutatua changamoto hiyo zikifanyika bila kuathiri utendaji wa halmashauri hiyo.



