TFS wahimizwa ubunifu, maadili

MOSHI, Kilimanjaro: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi amewaasa watumishi wapya wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuzingatia maadili, ubunifu na kufanya kazi kwa bidii wawapo kazini.

Katibu Mkuu ameusia hayo leo Aprili 08, 2024, katika Chuo cha Viwanda na Misitu (FITI) mjini Moshi alipofungua semina elekezi kwa watumishi 96 wa ajira mpya za TFS waliohitimu mafunzo ya awali ya uhifadhi na kuwa tayari kuanza majukumu yao kama watumishi wa umma.

“Pamoja na mambo mengine niliyowaeleza yatakayowasaidia kufika mbali suala la maadili ndio msingi mkuu. Mnakwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo mbalimbali ya misitu nchini ni matarajio yetu mtawahudumia wananchi na pale wanapokosea kuwaelimisha badala ya kutumia nguvu au kupokea rushwa kuacha raslimali zikiharibiwa. Binafsi nikisikia hayo kwenu nitasikitika sana na tutachukua hatua kali,” amesema Dk Abbasi.

Akiwa chuoni hapo pia ametembelea Chuo cha Viwanda na Misitu (FITI) na kuzungumza na wafanyakazi ambapo amewaeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inakijali mno Chuo hicho na mipango ya kukiboresha imeanza ikiwemo kuongezewa bajeti kwa zaidi ya asilimia 100 katika mwaka wa fedha utakaoanza Julai, 2024.

Habari Zifananazo

Back to top button