NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko leo Novemba 8 amemwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika sherehe za uapisho wa Rais wa sita wa Botswana, Gedion Duma Boko.
Uapisho huo uliofanyika katika Uwanja wa Taifa wa nchi hiyo umeshuhudiwa na mamia ya wananchi wa Botswana pamoja na wageni mbalimbali wakiwemo marais na viongozi wa wakuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Rais mteule wa Jamhuri ya Botswana ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Sita wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ambapo ameahidi kufanya kazi kwa kuzingatia misingi na sheria za nchi hiyo.
Aidha amesema atatekeleza majukumu yake ya kazi akijielekeza katika kuleta maendeleo na Usatawi wa Nchi na Wananchi wake.
Akihutubia taifa kwa mara ya kwanza Rais Boko amesema anajivunia taifa lake la Botswana huku akiongeza kuwa matokeo ya ushindi wake ni tukio la kihistoria kwake huku akiwataka wananchi wa Botswana kushikamana na kushirikiana katika kipindi kipya cha kisiasa ambacho amesema kinaongozwa na Amani, matumaini na kujijenga upya kijamii na kiuchumi.
SOMA: Dk Biteko amwakilisha Samia kamati kuu chama cha Kikomunisti
“Tarehe 30 Oktoba tulithubutu kupima demokrasia, amani na utulivu wa nchi hii na sasa najivunia kwamba tumeshinda mtihani kwa ushindi mkubwa” amesema na kuongeza kuwa matokeo hayo yatapimwa ustawi wake katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amesisitiza kuwa Botswana ni Jamhuri moja hakuna sababu ya kugawanyika bali umoja na mshikamano miongoni mwao na kusahau tofauti bali kuendelea kujenga kizazi kipya chenye matokeo makubwa zaidi ya sasa.
Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa dini katika hafla hiyo, wameliombea taifa hilo kuwa na umoja na mshikamano huku wakihamasisha msamaha miongoni mwa viongozi na wananchi wote pamoja na kuomba utendaji uliotukuka kwa Baraza la Mawaziri ili waweze kufanya kazi kwa kutetea rasilimali za nchi hiyo.