Dk Kasiluka ataka weledi ukagusi taasisi za umma

ARUSHA: KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt Mosses Kusiluka amesema kuwa wakaguzi wa ndani katika taasisi za umma na serikalini ni wataalamu muhimu sehemu yoyote na wanapaswa kufanya kazi kwa weledi katika majukumu yao ya kila siku ili serikali iweze kutekeleza kazi zake bila kuwa na changamoto zozote.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais –Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Juma Mkomi jijini Arusha kwa niaba ya Dk Kusiluka wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wakaguzi wa ndani uliohudhuriwa na Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi za umma,sekta binafsi na serikalini zaidi ya 400.
Mkomi alisema kuwa teknolojia imekuwa ikikua siku hadi siku hivyo wakaguzi wa ndani wanapaswa kubadilika na kwenda na wakati ikiwa ni pamoja na kuifanya kazi hiyo kwa weledi na umakini mkubwa lengo kuisadia serikali katika majukumu yake ya kila siku ya maendeleo.
Alisema Wakaguzi wa ndani katika taasisi za Umma ,sekta binafsi na serikalini wanapaswa kuifanya kazi hiyo kwa umakini na weledi ikiwa ni pamona na kuiboresha sekta hiyo ili iweze kuifanya kazi hiyo kwa uwazi na uwajibikaji uliotukuka na Wakurugenzi na wakuu wa taasisi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Wakaguzi hao wa ndani katika kutekeleza majumu yao ya kila siku bila ya kuwa na vikwazo vyovyote.
Alisema Wakaguzi wa ndani ni wataalamu waliobobea katika shughuli zao za kila siku na serikali inawajali na kuwathamni katika utendaji wao wa kila siku na ndio maana taarifa zao zinafanyiwa kazi pindi wanapoonyesha changamoto katika baadhi ya taasisi za umma,sekta binafsi na serikalini.
Mkomi alisema Wakaguzi wa ndani ni Wataalamu wanaotoa taarifa zao sahihi kwenye mamlaka husika kupitia mifumo ya Tehama na kama kutakuwa na wataalamu ambao sio sahihi serikali inaweza kuingia katika changamoto kubwa kwa kuwa inapata taarifa ambazo sio sahihi kitu ambacho anaamini mkuwa hakipo kwa sasa katika tasinia hiyo.
‘’Wakaguzi wa ndani ni idara muhimu katika taasisi za mumma na serikali hivyo wanapaswa kuifanya kazi hiyo kwa weledi na umakini mkubwa katika kuisaidia serikali ili iweze kufanya majukumu yake ipasavyo ’’alisema Mkomi
Naye Rais wa Wakaguzi wa Ndani Tanzania ( IIA ) Dkt Zella Njeza amesema kuwa lengo la Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wakaguzi hao ni kukumbushana juu ya ufanyaji kazi wa kila siku,utawala bora katika kazi na kuwakumbusha wakaguzi kufanya kazi kwa weledi na umakini lengo ni kuisadia serikali katika majukumu yake ya kila siku.
Dk Njeza alisema kuwa wako Arusha kwa siku tano na wameanza na wakurugenzi wa taasisi za umma,sekta binafsi na serikalini na mada mbali mbali zitajadiliwa lengo ni kuboresha utendaji kazi wa kila siku na kuangalia namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi lengo ni kutaka wakaguzi wa ndani kuifanya kazi hiyo kwa weledi.
Alisema kazi ya Wakaguzi wa Ndani ni kutaka taasisi za umma,sekta binafsi na serikali kufanya kazi kwa umakini na weledi ili serikali iweze kufanya kazi yake ipasavyo kwa maslahi ya nchini na sio vinginevyo.
Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Mstaafu ,Fredrick Utoh amesema kuwa IIA imekuwa ikifanya kazi zake vizuri toka ilipoanzishwa na kwa kiasi kikubwa imeisaidia serikali kutokuwa na changamoto nyingi katika taasisi umma ,sekta binafsi na serikalini.