Dk Kiruswa awataka Longido kumheshimisha Dk Samia

ARUSHA: MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk Steven Kiruswa amewaomba wananchi wa jimbo hilo kumheshimisha kwa kumpigia kura nyingi sambamba na mgombea urais wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendeleza zaidi maendeleo katika Jimbo la Longido.

Kiruswa amesema hayo katika vikao vya ndani vya kusaka kura kwa mbunge na rais katika Kata ya Kimokouwa, Engikaret na Longido vilivyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama ngazi ya matawi,kata na viongozi wa mila maarufu kwa jina la Laigwanani.

Amesema kuwa yeye kama mgombea ubunge angefurahi siku ya Oktoba 29 mwaka huu wananchi wa jimbo hilo ambao wengi ni wa jamii ya kifugaji kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura ili kumpa yeye kura nyingi na Rais kwa asilimia 99.

Amesema fadhila kubwa kwa wananchi wa Longido ni kumpa kura nyingi Rais kwani hiyo ndio itakuwa asante kwa kufanya mambo mengi ya maendeleo katika Jimbo la Longido kwani amewakomboa kwa kuwapelekea fedha nyingi za miradi ya maendeleo ikiwemo maji, afya, elimu na barabara.

Mgombea huyo amesema Longido wana sifa ya kumpa Rais kura nyingi mgombea urais wa CCM na kuongoza kimkoa na mwaka huu tunataka kuongoza Kitaifa kwa kumpa kura nyingi Rais kwani tunakila sababu ya kufanya hivyo kwa kuwa kila mwananchi analijua hilo,” amesema Kiruswa.

Naye, Mwenyekiti wa CCM Longido,Papa Nakuta amesema wananchi wa jimbo hilo wanakila sababu ya kumpa kura Rais na mbunge kwa kuwa miradi ya maendeleo iliyopelekwa Longido ina thamani kubwa kuliko miaka yote ya nyuma hivyo fadhila au asante ni kuwapa kura za kutosha wagombea hao.

Nakuta amesema kuwa katika nafasi ya udiwani kata zote 20 za jimbo hilo madiwani wote wamepita bila kupingwa katika kata zao na hakukuwa na wagombea wa vyama vya upinzani waliojitokeza kuwania nafasi na hiyo inatokana na jinsi jamii ilivyowakubali wagombea hao wa CCM.

Naye, Katibu Mwenezi wa CCM Longido,Solomoni Lekui aliwahimiza viongozi wa Mila na viongozi wenye ushawishi katika Jimbo la Longido kuhakikisha wanashawishi jamii hiyo ya kifugaji kujitokeza kupiga kura siku ya octoba 29 mwaka ili kutimiza malengo yao ya kuwachagua viongozi bora akiwemo Rais na mbunge ili waweze kuendeleza miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button