RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, DK Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada za kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii katika kipindi kifupi cha Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk Mwinyi ametoa pongezi hizo leo katika ufunguzi wa Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Swahili (8th edition of the swahili international tourism expo – s!te 2024) lililoanza leo Dar es salaam na kuwakutanisha wanunuzi wa bidhaa za utalii, waoneshaji, wawekezaji na wadau mbalimbali wa utalii wa ndani na nje ya Tanzania.
“Kutokana na juhudi hizo za Mheshimiwa Rais Dk Samia, idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea nchi yetu imekua kwa kasi sambamba na ongezeko la mapato yatokanayo na sekta ya utalii. Mathalan, hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 Tanzania imepokea jumla ya watalii wa kimataifa 2,026,378 ikiwa ni takwimu za juu kabisa kuwahi kufikiwa katika historia ya nchi yetu. Pia, mapato yatokanayo na sekta ya utalii yamefikia Dola za Marekani bilioni 3.5,” amefafanua Mwinyi.
Amesema sekta ya utalii imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania, huku ikichangia asilimia 17.2 ya Pato ghafi la taifa, asilimia 25 ya mauzo ya nje na kuzalisha ajira zaidi ya milioni 1.5 ikiwa ni ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia mnyororo wake wa thamani.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamewezesha nchi kutambuliwa kimataifa na kupata tuzo mbalimbali ambapo taarifa iliyotolewa mwezi Septemba, 2024 na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism – World Tourism Barometer) ambapo inaonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 6 duniani ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii.
Miongoni mwa tuzo hizo ni zile zilizotolewa mwaka 2023 na World Travel Awards (WTA) ambao wameitambua Bodi ya Utalii Tanzania kama Africa’s Leading Tourist Board, Kisiwa cha Thanda Shunghumbili, Mafia kama World Leading Exclusive Private Island, Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kama Africa’s Leading Tourist Attraction, na Hifadhi ya Taifa Serengeti kama Africa’s Leading National Park.
Aidha, mtandao wa Trip Advisor umezitambua Hifadhi za Taifa Serengeti na Tarangire kama Africa’s Top Attractions kwa mwaka 2023. Vilevile, Island Index wameitaja Zanzibar kuwa The 2nd Best Island Destination in the World kwa mwaka 2024.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi, Dk Pindi Hazara Chana wakati amemhakikishia Rais Dk Mwinyi kuwa wizara kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) itaendelea kutekeleza majukumu yake iliyopewa ya kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi sambamba na kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Utalii kwa kuzingatia Sera na miongozo mbalimbali.
Ametaja miongozo hiyo kuwa ni pamoja na Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999, Mpango Kamambe wa Utalii wa mwaka 2002, Ilani ya CCM kwa kipindi cha mwaka 2020 mpaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo, na Mkakati wa Kutangaza Utalii Kimataifa.
Amesema katika muktadha huo, mwaka 2014 Bodi ya Utalii Tanzania ilianzisha Onesho la Utalii la Kimataifa lijulikanalo kama Swahili International Tourism Expo (S!TE). Lengo la kuanzishwa kwa Onesho la S!TE ni kuwakutanisha watoa huduma waliopo katika mnyororo wa thamani wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi ambao hupata fursa ya kuonesha bidhaa mbalimbali za utalii.