Dk Mwinyi azindua Matumbaku Sports Complex

ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya nane inatilia mkazo ujenzi wa viwanja vya michezo mbalimbali ili kutanua wigo wa ajira kutokana na michezo pamoja na kuibua vipaji vya vijana.

Amesema azma ya Serikali ni kuendeleza michezo katika nyanja zote inatimia kwa kuweka miundombinu ya kisasa iliyobora na imara.

Dk Mwinyi amesema hayo Desemba 30, 2023 alipoufungua Viwanja vya Michezo vya Matumbatu ‘ Matumbatu Sports Complex’ uliopo Shehia ya Miembeni, Mkoa wa Mjini Magharibi katika shamrashamra za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Mwinyi amewatoa hofu wananchi wa Malindi kuwa dhamira ya ujenzi wa viwanja hivi ni kuwa mbadala maeneo yaliyofanyiwa uwekezaji.

Halkadhalika amewataka vijana watumie fursa za kuwepo kwa viwanja vipya vya kisasa kwa kuonyesha vipaji vyao ili waweze kutengeneza ajira ndani ya nchi na nje.

Pia amesema michezo ikitumika vizuri itakuwa ni fursa ya kuitangaza Zanzibar na kukuza utalii.

Advertisement

Eneo hilo lina viwanja vitatu vya mpira wa miguu, pamoja na kiwanja kimoja kwa michezo ikiwemo mpira wa wavu, mpira wa kikapu na netiboli.