Dk Mwinyi: Wapinzani hawana uwezo kuongoza

ZANZIBAR : MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema wapinzani hawana uwezo wa kuiongoza nchi. Dk Mwinyi alisema hayo wakati wa mkutano wa kampeni Pangawe juzi. “Nimekuwa nikiwasikiliza, sisikii sera hata moja. Sijawahi kusikia watafanya nini kwenye elimu, wala kwenye afya, barabara, viwanja vya michezo, wala kwenye maji.
Hakuna sera ndugu zangu, msije mkahadaika. Si watu wa kuchaguliwa, hawana uwezo wa kuongoza,” alisema. Aliongeza: “Ukitaka kujua tutashinda, tizama idadi ya watu wanaokwenda kwenye mikutano yao, halafu tizama ya kwetu. Hawatuwezi na hawatatuweza mpaka kiama,” Dk Mwinyi alisema serikali yake imetimiza ahadi zote za Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025 na hivyo kuwaomba wananchi wakipe ridhaa CCM, ili wafanye makubwa zaidi.
“Ninyi ni mashahidi. Mnaona kwenye eneo la elimu, ujenzi wa skuli mnaziona, afya ujenzi wa hospitali mnaziona za wilaya na mikoa. Kwenye barabara, barabara kuu za ndani mnaziona, kila mahali viwanja vya michezo vikubwa na vidogo mnaviona, masoko ya kisasa mnayaona kila siku mkipita barabarani.
Miradi ya umeme, maji ilimradi kila upande kuna miradi mikubwa inaendelea katika nchi yetu,” alisema. Dk Mwinyi alisema wananchi wakimchagua, atamaliza changamoto ya Barabara ya Pangawe kwa kuwajengea barabara za ndani kwa kiwango cha lami. Alisema katika elimu, anatambua changamoto ya shule za msingi za Tomondo, Uzi na Kinuni lakini tayari serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa shule mpya 29 za ghorofa, ili kukidhi changamoto katika maeneo hayo.
Kuhusu afya, Dk Mwinyi alisema serikali imeanza matayarisho ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kwarara Kidutani, ili kuondoa changamoto ya kituo cha afya katika eneo hilo. Kwenye viwanja vya michezo, Dk Mwinyi alisema serikali imeingia mikataba wa ujenzi wa viwanja 17 vya michezo. Pia, alisema serikali yake itaweka kipaumbele kwenye eneo la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kwa kutengeneza ajira serikalini, sekta binafsi na kutoa mikopo isiyo na riba kwa wajasiriamali.
“Tutatoa ajira serikalini, sekta binafsi ikiwemo viwanda lakini tutawawezesha wananchi kujiajiri wao wenyewe kwa kuwapa mikopo isiyo na riba,” alisema Dk Mwinyi. Awali, Dk Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetekeleza ahadi kwa wajasiriamali kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara, kwa kuwajengea masoko ya kisasa.
Alisema hayo alipokutana na wajasiriamali na wafanyabiashara wa Kibandamaiti. “Kwa upande wa wajasiriamali, tuliwaahidi tutawajengea mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao. Tumeendelea kujenga maeneo mbalimbali ya masoko, majiko na maeneo ya kufanyia biashara ili waweze kuwa na mazingira mazuri.

Kazi hii inaendelea Unguja na Pemba,” alisema Dk Mwinyi. Aliongeza: “Tumetekeleza sehemu kubwa ya haya, masoko tumejenga ya kisasa kabisa kama la Mwanakwerekwe, Jumbi, Chuwini na hivi karibuni litakamilika la Mombasa.” Pia, Dk Mwinyi alisema SMZ imetoa fedha za mikopo isiyo na riba kwa wafanyabiashara, wakulima wa mwani na wavuvi mikopo yenye thamani ya bilioni 96. SOMA: Dk. Mwinyi asema ahadi za serikali zinatekelezwa
Alisema SMZ imeondoa kero ya tozo zisizotabirika walizokuwa wanatozwa wafanyabiashara, akiahidi kwamba inaweza ikapunguzwa hapo baadae. “Tozo zimekuwa zinatabirika, sasahivi ni Shilingi 30,000 uongeze na 10,000 ya usafi na huko tunapokwenda tunaangalia uwezekano wa kupunguza, wafanyabiashara wasipate tabu ya kulipa fedha hizo,” alisema Dk Mwinyi.



