Dk Nchimbi aahidi pembejeo bure wakulima wa korosho

MTWARA: MGOMBEA Mwenza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi amesema serikali itaendelea kuwahudumia wakulima wa zao la korosho nchini kwa kuwapatia pembejeo za korosho bure.
Yamejiri hayo wakati alipohutubia wananchi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba, Tandahimba pamoja na Newala mkoani Mtwara kupitia mikutano ya kampeni iliyofanyika kwenye maeneo hayo kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
“Ruzuku ya mbolea na mbegu itaendelea kutolewa kwa wakulima wa zao la korosho pia itaongeza kiwango cha wingi wake na kutambuliwa ubora wake ili kuhakikisha wakulima wetu wanapata mbegu bora na mbolea bora,”amesisitiza Nchimbi
Ameongeza kuwa, “Ilani ya CCM imesema tutaendelea zaidi kuhakikisha kilimo chetu kwenye maeneo haya kinakuwa cha kutaalamu ili mazao yetu yaongezeke pia maofisa ugani wataongezewa uwezo wa kufanya kazi kwa kupatiwa mafunzo mengi”
Mbali na hilo amevitaja baadhi ya vipaumbele vya serikali katika kuwatekelezea wananchi kupitia Ilani ya CCM kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwemo ujenzi wa visima vipya vitakavyosaidia katika skimu za umwagiliaji kwenye maeneo hayo.
Aidha lengo la visima hivyo ikiwa ni pomoja na kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula katika maeneo hayo ili wakulima walime kisasa na kuongeza uzalishaji utakaowapelekea kupata fedha zaidi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara Saidi Nyengedi amesema taifa limewaheshimisha kwenye kanda hiyo ya kusini hivyo amemhakikishia mgombea huyo kuwa CCM itapata kura za kutosha katika uchaguzi huo.



