Tanzania yajitosheleza kwa chakula

MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amesema hatua kubwa zilizochukuliwa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha  kilimo cha kisasa zimeiwezesha Tanzania kujitosheleza kwa chakula na kuondokana na wimbi la uagizaji wa bidhaa za chakula kutoka nje.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jimbo la Kongwa mkoani Dodoma juzi jioni, Dk Nchimbi alisema mafanikio hayo yametokana na uamuzi wa serikali kuongeza bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Kilimo mara dufu, hatua iliyoleta mapinduzi makubwa katika uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara.

“Rais wetu Samia aligundua mapema kwamba zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, na asilimia 80 ya wananchi wa Kongwa ni wakulima. Ndiyo maana akaamua kuongeza bajeti ya kilimo, jambo lililoongeza tija katika sekta hii,” alisema Nchimbi.

Alibainisha kuwa kutokana na uamuzi huo, uzalishaji wa chakula nchini umeongezeka kutoka tani milioni 17 kwa mwaka hadi kufikia tani milioni 22, na hivyo Tanzania kuondokana na tatizo la upungufu wa chakula. “Hivi sasa Tanzania siyo tena kati ya nchi zinazohitaji msaada wa chakula. Tunajitosheleza kwa chakula chetu,” alisema Nchimbi.

Aliongeza kuwa katika kipindi kijacho cha miaka mitano, serikali imepanga kuimarisha zaidi skimu za umwagiliaji, kuhakikisha wakulima hawategemei mvua pekee, na kuongeza ruzuku za mbolea, mbegu na dawa kwa wakati pamoja na kuboresha huduma za ugani kwa wakulima wote.

Aidha, alisema serikali pia imeongeza idadi ya maofisa ugani na kuwapatia mafunzo na vitendea kazi vya kisasa ili kuhakikisha kilimo kinakuwa cha kitaalamu zaidi. SOMA: Samia aahidi kicheko kwa wavuvi

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button