Dk Netho apangua hoja za Polepole

IRINGA: Mtaalamu wa Uchumi, Utawala Bora na Siasa, Dk Netho Ndilito, amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ni Rais halali wa awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anayo haki ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza katika uchambuzi wake wa Katiba ya nchi, Dk Ndilito alisema kumekuwa na upotoshaji unaodai kuwa Rais Samia anaendeleza awamu ya tano ya urais iliyoanza na Hayati Dk. John Magufuli mwaka 2015.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 37(5) ya Katiba ya JMT, Rais Samia anatambuliwa kama Rais halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya kuapishwa kufuatia kifo cha Dk. Magufuli. Hivyo, alipotangaza kuchukua madaraka, alihesabiwa kama Rais wa awamu ya sita,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa hoja zinazodai Rais Samia hastahili kugombea urais mwaka 2025 kwa sababu aliingia madarakani mwaka 2015 si sahihi.
“Ibara ya 40(2) ya Katiba inaeleza wazi kwamba Rais anaweza kuchaguliwa kwa vipindi viwili tu vya miaka mitano mitano. Hivyo, muhula wa kwanza wa Dk. Samia ni 2020 hadi 2025, na anayo haki kamili ya kugombea muhula wa pili 2025–2030. Baada ya hapo, ataimaliza safari ya urais wa awamu ya sita,” alifafanua.
Dk Ndilito pia alikanusha madai kwamba viongozi waliowahi kushika nafasi za Makamu wa Rais au Waziri Mkuu hawaruhusiwi kugombea urais.
“Ni upotoshaji mkubwa. Dk Mohamed Shein aliwahi kuwa Makamu wa Rais na baadaye CCM ikampendekeza kugombea urais wa Zanzibar na akashinda. Hata hivyo, historia yetu inaonyesha wazi kwamba Mwalimu Nyerere kutoka nafasi ya Waziri Mkuu aliweza kuwa Rais, vivyo hivyo Mzee Cleopa Msuya alishawahi kugombea urais mwaka 1995 baada ya kuwa Waziri Mkuu,” alisema.
Kuhusu hoja zinazodai Rais Samia anaweza kuendelea kugombea hadi mwaka 2035, Dk Ndilito alisema:
“Hiyo si kweli. Katiba imetaja vipindi viwili pekee. Kwa maana hiyo, 2020–2025 ni muhula wa kwanza na 2025–2030 ni muhula wa pili na wa mwisho,” alisema.
Kuhusu tetesi kwamba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hakugombea ubunge kwa sababu Rais Samia hatomteua tena kuwa Waziri Mkuu, Dk Ndilito alifafanua kuwa ni umbea usio na msingi.
“Sio jambo jipya kwa Waziri Mkuu kumaliza muda wake na kubaki mbunge wa kawaida. Hali hiyo iliwahi kutokea kwa akina Cleopa David Msuya, Joseph Warioba na Edward Lowassa. Wakati mwingine kutogombea ni sawa na kustaafu au kuchukua mapumziko ya hiari,” alieleza.
Dk Ndilito alisisitiza kuwa ni muhimu Watanzania kufuata misingi ya Katiba na siyo maneno ya mitaani ambayo yanakusudia kuchafua taswira ya viongozi.



