Dk Netho: Polepole hafai hata kiongozi wa mtaa

Mtaalamu wa Uchumi, Siasa na Utawala Bora, Dk Netho Ndilito, ameendelea kujibu hoja zilizotolewa na aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, akizitaja kuwa zimejaa upotoshaji, chuki binafsi na mashambulizi yasiyo na msingi dhidi ya Rais, Dk Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza baada ya kufuatilia mahojiano ya Polepole yaliyosambazwa mitandaoni Agosti 29 majira ya saa tatu usiku, Dk Netho alisema mwanasiasa huyo alishindwa kusimamia hoja yake ya awali ya kupinga mchakato wa ndani wa CCM kumteua Dk Samia kugombea urais kwa muhula wa pili.
“Hapo mwanzo alitaka kuuaminisha umma kwamba uteuzi wa mgombea urais kupitia CCM haukuwa halali. Baada ya kubainika kwamba hoja zake hazina mashiko, ghafla akarukia mada nyingine ambazo nazo hazina uthibitisho wowote wa kikatiba wala kikanuni,” alisema Dk Netho.
Amemtaka Polepole kuuthibitishia umma katika awamu za pili za marais waliopita – Benjamin Mkapa mwaka 2000, Jakaya Kikwete mwaka 2010 na John Magufuli mwaka 2020 – zilitolewa fomu ngapi za uteuzi kwa wagombea, na kwaninini atake awamu ya pili ya Dk Samia ifanyike tofauti na desturi hiyo.
Kuhusu hoja ya kwamba urafiki wa Rais na wafanyabiashara ni tatizo, Dk Netho alisema:
“Kuongoza nchi si jambo rahisi. Marais kote duniani huwa karibu na wafanyabiashara ili kuchochea ukuaji wa uchumi. Uchumi ukiimarika, wananchi wa tabaka la kati na chini hunufaika kwa huduma bora. Tatizo liko wapi?”
Akizungumzia madai ya Polepole kuhusisha vifo vya baadhi ya viongozi waliotangulia mbele ya haki na mazingira ya kisiasa, alisema kitendo hicho ni cha kusikitisha na kinaweza kufikia kiwango cha jinai.
Alitoa wito kwa Jeshi la Polisi kumtaka Polepole kuwasilisha ushahidi wa madai yake.
Aidha, alimtuhumu Polepole kuwa na visasi na chuki binafsi, akidai kuwa kama ushauri wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete wa kutaka Polepole aondolewe katika nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ulikuwa ukweli, ulikuwa na mashiko.
“Polepole ndiyo uliyeua think tank ya CCM na akamuaminisha Rais aliyekuwepo kwamba yeye ndiye anayejua kila kitu, kumbe anampotosha,” alisema.
Dk Netho alihitimisha kwa kutoa rai kwa mamlaka za uteuzi kuhakikisha nafasi nyeti zinashikiliwa na watu wenye sifa, huku akiwataka Watanzania kuwapuuza viongozi wanaoendeleza siasa za maneno badala ya hoja zenye ushahidi.
“Polepole hana sifa za uongozi hata wa mtaa. Amejijengea utamaduni wa kupotosha na kufichua siri za chama na serikali kwa misingi ya upotoshaji. Ni wajibu wetu kumpinga kwa nguvu zote na kulinda heshima ya viongozi wetu wakuu,” alisisitiza.



