Dk Samia aahidi kuendeleza miradi Mtwara

MGOMBEA: Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendeleza miradi mikubwa ya kilimo na nishati mkoani Mtwara ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuboresha maisha ya wananchi.
Hayo yamejiri wakati alipohutubia mkutano wa kampeni uliyofanyika eneo la mangaka wilayani Nanyumbu mkoani humo.
Amesema serikali imepanga kukamilisha miradi ya visima vya umwagiliaji maji vya Likokona, Lukula na Masugulu ili kuongeza tija kwa wakulima na kuwawezesha kulima zaidi ya mara moja kwa mwaka.
“Serikali inaendelea kutafuta masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo ili kulinda bei za mazao makuu ya biashara hususan korosho, mbaazi, karanga na ufuta, ambayo kwa sasa yameonyesha ongezeko kubwa la uzalishaji”amesema Samia
Kwa upande wa nishati amebainisha mpango wa kujengwa kwa gridi imara ya umeme kutoka Songea–Tunduru hadi Masasi kwa gharama ya Sh bilioni 307.
Aidha mradi huo utahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kupooza na kusambaza umeme vitakavyowezesha wananchi pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji wa viwanda kupata nishati ya uhakika.
Mbali na hilo amewapongeza wananchi wa wilayani humo kwa kuutumia vyema mpango wa ruzuku ya mbolea na pembejeo za korosho uliyosaidia kuongeza uzalishaji wa korosho kutoka tani 15,000 hadi 24,000 na kuingiza zaidi ya Sh milioni 73 katika msimu uliopita mwaka 2024/2025.



