MWANASIASA Dk Wilbrod Slaa (76) amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shitaka linalomkabili la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa X kinyume na kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya kimtandao.
Hayo yalidaiwa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato, akisaidiana na mawakili wengine wa serikali, Tumaini Mafuru na Abdul Bundala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Akisoma mashitaka hayo, Kato alidai Januari 9, 2025 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia mtandao wa X wenye jina Maria Sarungi Tsehai, Slaa alisambaza taarifa kwa nia ya kuongopea umma wa Watanzania huku akijua kuwa taarifa hiyo ni uongo.
Kato alinukuu taarifa hiyo iliyoandikwa kwenye mtandao huo iliyosema:
“Wakubwa wametafutana, tukisema wakubwa tunamaanisha mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumumunya, Samia atatoa pesa kumsaidia Mbowe, hizo ni pesa za Watanzania wanazichezea, Samia na watu wake, Samia anahangaikia namna ya kurudi Ikulu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Dk Slaa.
Hata hivyo mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo.
Baada ya kusoma mashitaka hayo upande wa utetezi ukiongozwa na wakili, Hekima Mwasipu akisaidiana na Sanga Melkior waliomba mshitakiwa apewe dhamana kwa kuwa kosa hilo linadhaminika.
“Tunaomba mahakama yako tukufu impe mteja wetu dhamana yenye masharti nafuu, na tunaomba nafuu hizo ziwe ni katika namna ya kumfanya awe na haki ya kufanya kazi zake, na kusafiri,” alidai wakili Mwasipu.
Hata hivyo, upande wa mashitaka ulipinga ombi hilo na kudai tayari walishafaili kimtandao hati ya kiapo cha kuzuia dhamana kilichotolewa na SSP George Wilbard.
Nao, upande wa utetezi uliendelea kusisitiza ombi la mteja wao kupewa dhamana kwa kuwa walidai mchakato wa kiapo hicho haujawasilishwa kisheria.
“Kiapo hicho sisi hatujakiona, ni kama suala la kinadharia, halijafuata miongozo ya sheria na hivyo tunaomba mteja wetu adhaminiwe halafu upande wa Jamhuri waendelee na mchakato huo siku zijazo ili watupatie na sisi tuipitie tuone kama mteja wetu ana haki ya dhamana au hana,” alidai wakili Sanga.
Hakimu Nyaki aliahirisha shauri hilo hadi Januari 13, mwaka huu suala hilo la dhamana litakapojadiliwa mahakamani hapo.
Awali, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alithibitisha kukamatwa kwa Dk Slaa lakini hakuwa tayari kueleza kwa undani tuhuma zinazomkabili.
“Ni sahihi, Dk yupo na tupo naye tumekuwa na mahojiano naye kwa baadhi ya mambo na mahojiano yetu na yeye yanakwenda vizuri, kwa hiyo tunaangalia mifumo ya kisheria inatueleza nini cha kufanya zaidi na naamini taarifa zaidi zitatolewa baadaye,” alisema Muliro.
Dk Slaa alikamatwa usiku wa kuamkia jana Januari 10, 2025 nyumbani kwake Mbweni.
Dk Slaa, aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mbunge wa Karatu na Balozi wa Tanzania nchini Sweden.