Dk Tulia amlilia Ndugai, ataka viongozi waache alama

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson ametoa mwito kwa viongozi watumie mamlaka waliyopewa kuacha alama ya mafanikio.
Dk Tulia alisema hayo wakati wa ibada ya kuuaga mwili wa Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana.
Alisema maisha ya Ndugai yalikuwa ya huduma ya kujitolea na ameacha alama isiyofutika katika taifa.
“Alikuwa mwalimu bora na mwema kwangu, mara zote alinisisitizia kwamba tunapaswa kuwa na Bunge imara linaloishauri na kusimamia serikali kwa uwazi kwa maslahi ya wananchi na si kwa kelele bali kwa hoja na mafanikio na kauli hizo zilikuwa dira kwa malengo waliyojiwekea na kuhakikisha serikali inaendelea kuwezesha ustawi wa wananchi wote,” alisema Dk Tulia.
Alisema Ndugai alikuwa zaidi ya kiongozi wa kisiasa, mwalimu wa nidhamu, mlezi wa mshikamano, mtetezi dhabiti wa haki na alielewa kwa undani kwamba uongozi si heshima ya vyeo bali ni wito na wajibu wa kujitoa kwa dhati kwa ajili ya wengine.
“Job Ndugai pumzika salama kiongozi wetu, mlezi wetu, rafiki yetu, baba yetu, mpendwa wetu na ndugu yetu kama ulivyopenda kutuita ndugu zako katika miaka 25 uliyolitumikia Bunge,” alisema Dk Tulia.
Alisema Ndugai aliyaishi maandiko ya Mungu ambayo yanasema kama mtu anataka kuwa wa kwanza na awe mtumishi wa wote na maneno hayo hakuyatumia kama falsafa yake bali aliyatekeleza kwa vitendo.
Dk Tulia alisema watu wengi wameshuhudia mema ya Ndugai kipindi alichowaongoza hivyo waomboleze kwa kuendelea kumsikiliza na kujifunza kutoka kwake na kukumbuka mchango mkubwa aliofanya kwa Bunge na wananchi wa Jimbo la Kongwa na Tanzania.
Alisema Ndugai alikuwa mbunifu aliyeleta mageuzi ya kiutendaji ndani ya bunge hasa kipindi ugonjwa wa Covid 19 ambapo alikuja na ubunifu wa uendeshaji wa shughuli za bunge kwa njia ya mtandao na ubunifu huo umefanya hadi leo Bunge kuacha kutumia karatasi.
Pia, alisema Ndugai ndiye aliyepeleka wazo la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Dodoma iliyopewa jina la Bunge ambayo aliisimamia kuhakikisha shule hiyo inajengwa na tayari Bunge limeanza utaratibu wa kujenga Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Bunge.
Alisema kiongozi huyo alisimamia kutungwa sheria ikiwemo ya uanzishaji wa makao makuu ya nchi kuwa Dodoma ya mwaka 2018 ambayo imefanya maendeleo yote yanayoendelea kufanywa Dodoma yawe makamilifu.
Alisema Ndugai alikuwa kiongozi mwenye roho ya kulea na wabunge wapya walimuona kama mwalimu.
Dk Tulia alisema wabunge walipopitia changamoto walimuona kama ndugu mwenye busara na mwenye msaada wa dhati hivyo watamkumbuka kama mtu mwenye msimamo dhabiti aliye waonyesha kuwa mamlaka wanayoshikilia si yao binafsi bali ni amana kutoka kwa Mungu.
“Alipambana na utovu wa nidhamu kwa kusimamia kanuni bila kupendelea na alikuwa mstari wa mbele katika kutafuta maeneo ya maridhiano ya kisiasa ili kuhakikisha mshikamano ndani ya Bunge na kitaifa,” alisema Dk Tulia.