‘Drones’ kuongeza ufanisi kwa wakulima

WAKULIMA wamepewa taarifa njema ya ujio wa teknolojia ya kisasa ya ndege nyuki ‘drone’ kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika sekta ya kilimo nchini. Hatua hii inalenga kuongeza tija, kupunguza gharama na kurahisisha kazi kwa wakulima na taasisi mbalimbali nchini.
Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Mati Group of Companies, David Mulokozi, amesema kampuni hiyo imeamua kuwekeza kwenye teknolojia ya drone zitakazotumika kunyunyizia dawa mashambani, kupima maeneo, kupanda mbegu, kusafirisha mizigo, kusaidia kaguzi mbalimbali nk.
Mulokozi ameeleza kuwa ‘drone’ hizo zinazotengenezwa ndani ya nchi zitauzwa kuanzia Sh milioni 17 kulingana na mahitaji ya mteja, hali itakayowawezesha wakulima wengi kuzimudu kulinganisha na gharama kubwa za uagizaji bidhaa hizo nje ya nchi.

“Tunaendelea na mazungumzo na benki mbalimbali ili ziweze kuwapatia wakulima mikopo ya kupata ‘drone’ hizi kwa ajili ya kuimarisha shughuli zao za kilimo,” alisema.
Aidha, amebainisha kuwa uzalishaji wa ‘drone’ hizo ndani ya nchi utatoa ajira kwa wahandisi wa Kitanzania, huku wachache kutoka nje wakihusishwa katika programu za mafunzo na uhamishaji wa teknolojia.
“Tumeona changamoto kubwa inayowakabili wakulima hasa kwenye unyunyiziaji wa dawa, jambo linalopoteza muda na kuhatarisha afya zao, kwa drone hizi, hekari moja inaweza kunyunyiziwa dawa ndani ya dakika saba tu,” aliongeza Mulokozi.

Ofisa Ushirika kutoka Ofisi ya Msajili Mkoa wa Manyara, Godamen Merinyo, amesema teknolojia hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wakulima, hususan katika mazao kama mbaazi ambayo mara nyingi hukua kwa urefu na kufanya upuliziaji wa dawa kuwa ngumu na wa gharama kubwa.
“Hii itasaidia kuongeza uzalishaji kwa gharama nafuu na kuimarisha vyama vya ushirika, sisi kama viongozi wa ushirika tutaanza kutoa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia hii,” alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa mkoa wa Manyara, Paulo Eugine, amesema ‘drones’ hizo zitasaidia kuwalinda wakulima dhidi ya madhara ya kiafya yaliyokuwa yanawapata kutokana na kutumia pampu za mgongoni. “Sasa mkulima ataweza kutumia remote control bila kuingiliwa na sumu, jambo linaloimarisha usalama na afya zao,” alisisitiza.
Hatua hii ya Mati Technology inatarajiwa kuwa chachu ya mapinduzi ya kilimo nchini, sambamba na kuunga mkono jitihada za serikali katika matumizi ya teknolojia za kisasa kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo.



