EAC, SADC msikate tamaa amani DRC

HIVI karibu askari wawili wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) walipoteza maisha katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda aliwasilisha salamu za rambirambi na ubani kwa familia ya askari waliopoteza maisha wakilinda amani nchini humo.

Walikuwa DRC ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kushiriki ulinzi wa amani.

Walipoteza maisha kutokana na mapigano baina ya kikundi chao na kundi la M23.

Kimsingi, ni utaratibu wa Tanzania kupeleka askari wake katika nchi ambazo amani inatetereka na wanakwenda chini ya mwavuli wa ama Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) au EAC.

Askari wengine wapo katika nchi za Lebanon, Afrika ya Kati, Msumbiji na Congo. Tunalipongeza JWTZ kwa ujasiri na uzalendo wake kwa Afrika na kuendelea kuhakikisha linatoa mchango wa hali na mali kulinda na kudumisha amani miongoni mwa nchi za Afrika.

Hii inatukumbusha ukweli kuwa, ‘binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.’

Kadhalika, tunazipongeza nchi zote zinazojitoa kupeleka askari wake kusaidia ndugu zetu katika nchi zenye tabu kwa kuwa nyingine licha ya kuwa na changamoto kukosa amani, pia zinateswa na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi na magonjwa mbalimbali.

Tunaamini kuwa, changamoto iliyotokea kwa askari hao si tu kwao pekee, bali huwafika hata wengine miongoni mwa
nchi hizo zinazojali udugu.

Wakati Watanzania, wanaEAC na watu wa nchi za SADC wakizidi kuwaombea kila la heri, tunawapa moyo JWTZ katu isikate wala kukatishwa tamaa kwa hatua hii njema wanayofanya.

Aidha, tunahimiza watu wa nchi zenye changamoto ya amani kulinganisha faida na hasara waipatayo kwa ‘kumwagiana damu’ eti kwa sababu tu ya madaraka ambayo katika hali ya kawaida, uongozi na madaraka hutoka kwa Mungu.

Umefika wakati kila upande unaohusika, kunuia kwa dhati kukomesha uhasama huo baina ya ndugu na ndugu,
huku wakizingatia kuwa wapo baadhi ya watu au mataifa wanaoshangilia maana wanajua ‘vita ya panzi ni furaha kwa
kunguru.’

Hao wanapenda uhasama huo uendelee ili ama wazidi kuuza silaha au kuhujumu rasilimali za nchi kwa kujinufaisha wao.

Kadhalika, viongozi na wakuu wa nchi hizo, EAC, SADC na Afrika kwa ujumla wazidi ‘kukuna vichwa’ wakimwomba
Mungu wapate ufumbuzi wa migogoro hii ambayo pamoja na kwamba ipo kwenye nchi hizo, lakini inaathiri ukanda na Afrika kwa ujumla.

Ndio maana tunasema EAC, SADC msikate tamaa kuhusu suala la amani DRC maana Mungu yupo pamoja nanyi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button