Elimu jinsi ya kufikia ustawi wa kifedha

WATU wengi wanapofikiria kuhusu ustawi wa kifedha, mawazo yao huenda moja kwa moja kwenye kipato: Je, ninapata kipato cha kutosha? Je, ninaweka akiba ya kutosha? Lakini ustawi wa kifedha ni zaidi ya hayo.
Ni hali ya kuwa na usalama wa kifedha, uwezo wa kukabiliana na mambo yasiyotarajiwa, na maandalizi ya maisha ya baadaye.
Kuna misingi mitatu muhimu inayosaidia kujenga uthabiti wa kifedha. Habari njema ni kwamba misingi hii si migumu na wala haihitaji gharama kubwa.
Msingi wa kwanza ni kulinda kipato chako. Kwa watu wengi, uwezo wa kufanya kazi na kupata kipato ndicho kinachowezesha maisha kuendelea—kulipa ada, kuweka chakula mezani na kugharamia mahitaji ya kila siku.
Hata hivyo, maisha hayawezi kutabirika. Magonjwa, ajali au changamoto nyingine zinaweza kuvuruga mwenendo huu. Hivyo basi, ulinzi wa kipato ni jambo la msingi.
Bima ya maisha ina mchango mkubwa katika kulinda kipato chako. Si tu kwa ajili ya kujiandaa na yasiyotarajiwa, bali pia kwa kusaidia familia yako kifedha na kuwapatia amani ya moyo katika nyakati ngumu.
Pili ni kupangilia matumizi na kudhibiti madeni. Hapa ndipo watu wengi hukwama. Ni rahisi kutumia zaidi ya unachopata au kukopa kupita uwezo, hasa kutokana na mashinikizo ya maisha ya kisasa.
Ni muhimu kuwa na bajeti rahisi, kufuatilia matumizi yako, na kutanguliza mahitaji muhimu. Madeni si mabaya endapo yamechukuliwa kwa malengo ya msingi na kuwepo mpango wa namna ya kuyalipa.
Msingi wa tatu ni kupanga kwa ajili ya baadaye.
Hili lina maana tofauti kwa kila mtu—kuanzia kustaafu, kugharamia elimu ya watoto, kumiliki nyumba au kuanzisha biashara ndogo. Huna haja ya kuwa na fedha nyingi ili uanze kupanga. Hatua ndogo na endelevu kama kuweka akiba mara kwa mara au kuwa na mpango wa bima ya muda mrefu vinaweza kukusogeza karibu zaidi na malengo yako.
Kwa upande wa kampuni ya Jubilee Life Insurance, inaamini kwamba kila mtu anastahili kuishi kwa amani ya moyo na kujiamini. Kampuni inahakikisha inakuwa pamoja na mteja katika safari ya maisha kwa kumpatia mwongozo na nyenzo zitakazomsaidia kulinda kile kilicho cha muhimu zaidi kwake.
Kuwa na malengo ya kifedha haina maana kuwa kila kitu kipo sawa. Bali ni kuchukua hatua sahihi leo kwa ajili ya kesho yenye utulivu Hillary Godson ni Mhasibu Mkuu wa Jubilee Life Insurance Corporation of Tanzania Limited