Ewura yasisitiza usahihi uuzaji bidhaa

ARUSHA: Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) nchini Tanzania imewataka wafanyabiashara kuendelea kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu kwa kuuza bidhaa kwa usahihi kwa mujibu wa masharti ya leseni zao.
Meneja wa EWURA, Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Lorivii Long’idu amesema hayo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Arusha ambapo mamlaka hiyo imefika kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya taasisi hiyo inavyofanya kazi katika udhibiti wa bidhaa inazozidhibiti.
Amesema EWURA ni mdhibiti wa masuala mazima ya maji, mafuta kwa ajili ya magari na kuendesha mitambo, umeme,gesi pamoja na usafi wa Mazingira.
“Tumejikita katika maeneo mawili makubwa ambayo ni ya kiufundi na kiuchumi. Katika masuala ya kiuchumi tunaangalia sana huduma hizi kuwa zinatakiwa kupatikana kwa usahihi na kwa gharama ambayo mwananchi anaweza akaimudu pia kuhakikisha huduma hii inakuwa endelevu,”amesema Long’idu.
Amesema wafanyabiashara wanaouza mitungi ya gesi waendelee kuzingatia sheria taratibu na kanuni ikiwemo kuuza mitungi yenye kiwango cha gesi sahihi na siyo zilizochakachuliwa na pia ziuzwe kwa mwananchi kwa ubora ule ule uliothibitishwa .
Amesema EWURA inachakata bei za bidhaa ambazo wanazidhibiti ikiwemo utoaji wa bei za mafuta mara moja kila mwezi lengo ni kuhakikisha mwananchi anapata bei sahihi lakini pia mtoa huduma anaweza kutoa bei sahihi bila kutetereka na akahamasishwa sana katika uwekezaji .
“Huduma za mafuta zimeendelea kuimarika hapa nchini ,ujenzi wa vituo vya mafuta ambavyo viko katika viwango bora kabisa vinaendelea kuongezeka na hii maana yake sisi kama wadhibiti tumeendelea kumlinda mwekezaji pia kumlinda mwananchi kuhakikisha anapata bei ambayo ni himilivu,”ameongeza.
Amefafanua kuwa,EWURA imeendelea kuhakikisha kuwa bidhaa zinauzwa kwa bei iliyowekwa na EWURA na wanatembea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya mafuta kuona ubora na uuzwaji unafanyika katika miundombinu ambayo ni salama.
“Kama EWURA tunajikita kuhakikisha hakuna majanga yoyote yanaweza kutokea na kuleta athari kwenye mazingira, afya au usalama katika maeneo hayo na ndio maana tumekuwa tukikagua na tukikuta kituo hakikidhi ubora huwa tunakifunga hivyo hivyo katika masuala ya maji na usafi wa mazingira tunaendelea kuona uimarikaji na upatikanaji wa huduma na kama wadhibiti tunazisimamia kuhakikisha wanatoa huduma kwa bei sahihi na kwa wakati,”ameeleza.
Amesema wananchi wanapopata changamoto katika maeneo ambayo wanayasimamia wafike katika mamlaka hiyo na yatafanyiwa kazi na haki zao zitapatikana pia amewasihi kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia kama ilivyoelezwa kwenye Mkakati wa serikali wa Nishati Safi ya kupikia unaolenga ifikapo 2034 zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi na salama.