Fadhili Ngajilo ajitosa ubunge Iringa Mjini ataja ahadi 10 mageuzi

IRINGA: KATIKA hatua inayoakisi mvutano wa kisiasa unaotarajiwa kushika kasi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa na Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni ya VunjaBei, Fadhili Ngajilo, ametangaza rasmi nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia chama chake.

Akizungumza mbele ya wanahabari leo mjini Iringa, Ngajilo alisema amejipanga kwa nguvu mpya kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine, akiahidi kushughulikia changamoto za kijamii, kiuchumi, na kisiasa zinazolikumba jimbo hilo. Azma yake inakuja katika kipindi ambacho mchuano wa kisiasa ndani ya CCM unaanza kuchukua sura ya ushindani wa hali ya juu.

Ngajilo si mgeni katika medani ya siasa za ndani ya chama. Alishawahi kuwania ubunge kupitia CCM mwaka 2010 na 2015, na sasa anarudi tena mwaka huu akiwa na rekodi ya kuleta upinzani mkubwa ndani ya kura za maoni.

Akitangaza nia hiyo, alisema tayari ameandika barua ya kupisha kwa muda nafasi yake ya uenyekiti wa wazazi ili kutoa nafasi kwa vikao vya uchaguzi kufanyika kwa haki na usawa.

Wanane wajitokeza ubunge jimbo la Wete

“Ni matumaini yangu kuwa chama changu kitaona dhamira yangu ya dhati na wanachama wenzangu watanipa ridhaa. Ninaamini pia wananchi wa Iringa Mjini watanipokea kama mtumishi wao wa kweli,” alisema Ngajilo.

Katika mkutano huo na wanahabari, Ngajilo aliwasilisha vipaumbele kumi ambavyo vitakuwa dira ya utendaji endapo atapewa ridhaa ya kuwa Mbunge wa Iringa Mjini.

Alisema lengo lake kuu ni kuwa “sauti ya wananchi” itakayosikika kitaifa, hasa bungeni, na kuvutia maendeleo ya kweli kwenye sekta za kilimo, biashara, ajira, elimu na afya.

Akiwa na maono ya kiuchumi, Ngajilo alisema: “Vita vya kiuchumi vinahitaji hoja na uwezo wa kuvutia wawekezaji. Sauti yangu itawakilisha wakulima, wajasiriamali, vijana na wanawake wa Iringa mjini katika kila ngazi.”

Aliwahakikishia wajasiriamali kama machinga, mama na baba lishe, bodaboda, bajaji, mafundi na wafanyabiashara wa masoko kuwa atakuwa mtetezi wao mkuu kwa kuweka mifumo ya kusaidia shughuli zao kustawi.

Ngajilo alisisitiza umuhimu wa kuunganisha vyuo vikuu vya Iringa na jamii, kwa kuona wanafunzi kama rasilimali ya maendeleo ya mkoa huo.

Aliahidi pia kushughulikia changamoto za kiusalama zinazowakumba watoto, wanawake na wazee kwa kushirikisha jamii nzima katika kujenga mfumo madhubuti wa ulinzi wa kiraia.

Ngajilo pia amejitambulisha kama mlezi wa michezo akijivunia mashindano ya Ngajilo Cup (VunjaBei Cup) yanayoshirikisha vijana wa Iringa kupitia taasisi ya Ngajilo Foundation.

“Iringa tunahitaji timu ya Ligi Kuu. Nipo tayari kulipigania hilo,” aliahidi.

Katika sekta ya utalii, alieleza kuwa Iringa Mjini ina hazina kubwa ya vivutio vya kipekee, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na mandhari ya kuvutia ya mkoa.

“Uwanja wetu wa ndege, hali ya hewa na ukarimu wa wana Iringa ni vivutio tosha vya kuwafanya watalii wawe sehemu ya maendeleo ya Iringa,” alisema.

Katika maeneo ya pembezoni mwa mji, Ngajilo alisema bado kuna changamoto za barabara, huduma za afya na elimu, ambazo zinahitaji msukumo mpya kutoka kwa mbunge anayejua kusukuma ajenda bungeni kwa ufanisi.

“Nina maono, uzoefu na moyo wa utumishi wa kweli. Nataka kuwa mtumishi wa watu—na kuwatumikia wana Iringa Mjini kwa heshima na uadilifu.

Kwa kupitia azma yake hiyo, Ngajilo anaingia rasmi kwenye orodha ya wana CCM wanaowania tiketi ya kugombea ubunge katika moja ya majimbo yenye ushindani mkali nchini, jimbo ambalo limekuwa na historia ya mabadiliko ya uwakilishi wa mara kwa mara kwa miongo miwili iliyopita.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button