FCC yahimiza akili unde kukuza uwekezaji

TUME ya Ushindani (FCC) imesema akili unde ikitumika ipasavyo italeta tija ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani yenye kaulimbiu isemayo: ‘Akili Mnemba, Walaji na Sera za Uchumi’ yaliyoanza Disemba 1 na kilele chake kikitarajiwa kufanyika Dar es Salaam, Desemba 5, mwaka huu.
“Teknolojia hii inaweza kukuza kwa haraka ubunifu na maendeleo, mfano kusaidia kampuni shindani kuweka kipaumbele katika tafiti (R&D) ili kuweka mifumo rahisi na kusaidia uvumbuzi kwa haraka katika ufanyaji biashara, kupunguza gharama za uendeshaji kwa ufanisi na kuwa na ushindani wa bei au kutoa huduma bora,” alisema Khadija.
SOMA: FCC yatakiwa kudhibiti bidhaa feki
Aliongeza: “Matumizi ya Akili Unde yanachochea ushindani kati ya kampuni tofauti na kusababisha kutafutwa kwa masoko mapya yakiwemo ya kilimo, afya, fedha na elimu. Hii teknolojia husambaa kwa jamii nzima na si kwa wataalamu wachache hivyo kuwa na manufaa mapana kwa jamii na kuongeza chachu kubwa katika uchumi wetu na itasaidia vijana fursa za kutumia teknolojia hiyo kujikwamua kiuchumi.”
Alisema kaulimbiu ya mwaka huu imekuja wakati muafaka kwa sababu pamoja na mambo mengine Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mifumo katika ufanyaji kazi na kuwahudumia wadau wao.
Khadija alisema teknolojia, matumizi ya Tehama na mifumo inakua kwa kasi, hivyo FCC haina budi kuhakikisha inaangalia vizuri matumizi ya Akili Unde katika kusimamia soko la ushindani nchini.
“Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na teknolojia nyingi zinazotumia Akili Mnemba ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaweza kuathiri soko la ushindani kwa kusababisha uvujaji wa siri za kibiashara, taarifa zisizo rasmi, upendeleo wa algorithmic, utapeli, kuvaa wasifu wa mtu mwingine, usalama na uhakika wa mienendo ya kibiashara,” alisema.
Khadija alisema katika kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa haki, FCC pamoja na mambo mengine hushiriki
kuzuia makubaliano yanayofifisha ushindani baina ya washindani kwa kupangaji wa bei usiofaa ama kushusha bei kupita kiasi ili kuua ushindani.
Aliongeza kuwa jambo jingine ni kuzuia matumizi mabaya ya nguvu ya soko ikiwemo kizuizi dhidi ya washiriki wengine na wapya katika biashara au huduma kwa kutumia mbinu kandamizi zinazolenga kuwaengua au kuwadidimiza washindani katika biashara.
Aidha, alisema wanadhibiti miungano ya kampuni inayofifisha ushindani ikiwemo kuhakikisha kampuni zote zinazotoa huduma ama zinazozalisha mali zinatakiwa kuitaarifu FCC kuhusiana na kusudio la kuunganisha shughuli zao za kibiashara.
“Hili linafanyika ili kampuni moja inaponunua hisa za kampuni nyingine au kuinunua kampuni kusiwepo na
ukiritimba unaoweza kutokea baada ya muungano huo,” alisema.



