Gari lateketea moto, 6 wafa

RUVUMA; WATU sita wamefariki dunia baada ya gari dogo aina ya Prado lenye namba za usajili T647 CVR walilokuwa wanasafiria kutoka Kijiji cha Lumalu, Kata ya Upolo kwenda Kilosa, Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, kuanguka na kuteketea kwa moto katika mteremko mkali wa Chunya wilayani Mbinga kabla ya kufika mpakani mwa Wilaya ya Mbinga na Nyasa.
Waliopoteza maisha ni walimu wanne wa Shule ya Msingi Lumalu, Kata ya Upolo, mfamasia na dereva wa gari ambaye ni mume wa mmoja wa walimu hao na wote majina yao bado hayajafahamika.
Watu hao walikuwa wanakwenda Shule ya Sekondari Limbo wilayani Nyasa kwa ajili ya kufanya usaili wa watendaji na uboreshaji wa upigaji kura, utaratibu uliofanyika jana wilayani Nyasa na inaelezwa kuwa katika shule waliotoka walimu hao na kuwa amebaki mwalimu mmoja tu ambaye alikuwa likizo.
Akizungumza katika eneo la ajali, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyasa, Salum Ismail kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Peres Magiri alisema kuwa miili ya watu hao imepelekwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga ambako ni karibu zaidi ikilinganishwa na Nyasa kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Ismail aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza haraka katika eneo la ajali kwa ajili ya kutoa msaada na kuwaomba kuendelea na tabia hiyo pindi zinapotokea ajali kwenye maeneo yao.
Aliwaomba ndugu na jamaa kufika katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga (Mbuyula) kwa ajili ya kupima Vinasaba (DNA) ili kuwatambua wapendwa wao kwani hadi sasa watu hao hawajafahamika kutokana na kuteketea vibaya na moto.
Baadhi ya mashuhuda walisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva kushindwa kulimudu gari kutokana na kona kali baada ya kugonga kingo za barabara kabla ya kuanguka.
“Hii barabara haihitaji madereva wenye mbwembwe au magari mabovu kutokana na kuwa na kona nyingi na miteremko, lazima dereva awe mzoefu wa kupita mara kwa mara ili kunusuru maisha yake na watu anaowabeba,” alisema John Kapinga, mkazi wa Kijiji cha Buruma wilayani Mbinga.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri alithibitisha na kuwataja waliokufa kuwa ni Vincent Milinga (dereva) na walimu, Damas Nambombe, Dominica Ndau, Judith Nyoni na John Mtuhi pamoja na Boniface Mapunda (raia)



