Geita wajipanga kulinda hadhi ya manispaa

MBUNGE wa Geita mjini, Costantine Kanyasu amesema kuwa mara baada ya halmashauri hiyo kupandishwa hadhi kuwa Manispaa, mpango uliopo sasa ni kuhakikisha miradi yote inazingatia Mpango Mkuu (Master Plan).

Kanyasu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wadau wa vyombo vya habari wilayani Geita na kueleza miongoni mwa kikwazo kikubwa kilichochelewesha Geita mji kuwa Manispaa ni ujenzi holela.

Amesema mpaka sasa zaidi ya asilimia zaidi ya 60 ya eneo la manispaa ya Geita limejengwa bila kupimwa na kuzingatia mipango miji ambapo tayari wameweka mkakati wa kupima eneo lote na kukamilisha Mpango Mkuu.

Advertisement

“Ukifuatilia hotuba zangu bungeni niliwahi kusema sisi ni halmashauri ya mji yenye mapato makubwa kuliko mikoa mingi, kwa hiyo hakukuwa na sababu ya kuinyima manispaa”, amesema Kanyasu.

Amesema manufaa makubwa ya Geita mji kuwa Manispaa ni kusaidia mpango wa halmashauri hiyo kuweza kufikia hadhi ya jiji la Geita kwa kuongeza bajeti ya miundombinu bora ya barabara za kisasa hasa lami.

“Lakini pia tutapandisha hadhi ya huduma mbalimbali, kutaongeza thamani ya aridhi, viwanja vikipimwa ukiwa halmashauri ya mji bei yake ni ndogo, ikija manispaa inapanda, ikija jiji inapanda zaidi.

“Kuna miji mingine kiwanja kinauzwa mpaka milioni 600, siyo kwa sababu ni ghali ni kwa sababu upo kwenye manispaa au upo kwenye jiji, kwa hiyo thamani ya aridhi inapanda, huduma zinapanda viwango”, amesema.

Kanyasu amewataka wakazi wa manispaa ya Geita kuhakikisha wanalinda maeneo yao na kuachana na uuzaji holela wa viwanja vyao ili waweze kunufaika moja kwa moja na hadhi ya manispaa.

MWISHO