Geita yafungua milango ujenzi mabanda viwanja vya Samia
MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ametangaza kuwa milango ipo wazi kwa wadau mbalimbali kuanza ujenzi wa mabanda ya kudumu katika viwanja vya Maonyesho ya Madini (Viwanja vya Samia) mkoani humo.
Shigela ametoa tangazo hilo mbele ya wajumbe wa kikao cha Kamisheni ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kueleza hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
Oktoba 13, 2024, Rais Dk Samia aliagiza mkoa kuratibu ujenzi wa mabanda ya kudumu kwenye viwanja hivvo vilivyopo eneo la Bombambili mjini Geita wakati akifunga maonyesho ya saba ya Teknolojia ya Madini.
Shigela amesema hatua hiyo itapunguza gharama za maandalizi ya maonyesho ya madini kwani mpaka sasa kila mwaka mkoa unatumia zaidi ya sh milioni 300 hadi 400 kwenye ukodishaji wa mahema.
“Ili kupunguza gharama za kila mwaka kuandaa mabanda ya maonyesho, tuliazimia na tuliagizwa tuanze kujenga miudombinu ya kudumu kwenye eneo la maonyesho yetu.
“Sasa tumeshaandika barua kuzikumbusha mamlaka, taasisi, sekta binafsi, wote walioshiriki maonyesho na wanaotaka kushiriki, waje wapewe maeneo waanze ujenzi.
“Tulikubaliana mwisho wa Machi 31 2025 ndio kikomo cha uthibitisho kwa wanaotaka kujenga miundombinu ya kudumu kwenye uwanja wa maonyesho”, amesema Shigela.
Amesema kwa taasisi au wadau ambao hawatathibitisha kwa wakati kamati ya ugawaji maeneo ambayo ipo chini ya mkuu wa wilaya, wakurugenzi na wabunge itagawa maeneo kwa watu walio tayari.
Aidha ameelekeza ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita kuandaa bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya kudumu kwenye eneo hilo.
Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba amesema mradi wa ujenzi wa mabanda ya kudumu katika viwanja vya Samia utaanza kutekelezwa kwa makundi mawili, kwanza ni kwa fedha zilizotokana na maonyesho ya mwaka 2024 na pili ni kwa fedha za wadau walio tayari.
“Tuna maeneo pale kwa ajili ya taasisi za serikali, nilikuwa naomba wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri wanaporudi kwenye maeneo yao wajue kabisa wana wajibu wa kutenga bajeti katika hili”, amesema.



