Gerema yaonya wachochezi migogoro migodini

SHIRIKISHO la Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Geita (GEREMA) limewaonya watu wenye tabia ya uchochezi wa migogoro kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo kuacha mara moja kwani wanaminya fursa za wachimbaji wadogo.

Mwenyekiti wa Gerema, Titus Kabuo ametoa kalipio hilo juzi wakati akizungumza na wachimbaji wadogo katika mgodi wa Ililika uliopo kata ya Nyarugusu wilayani Geita alipofika kutatua changamoto cha wachimbaji hao.

Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu inafanya kazi kubwa kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo hivo Gerema haitamvumilia mtu yeyote anayekwamisha maendeleo ya wachimbaji wadogo Geita.

Amesema mgogoro kimaslahi ulitokea mgodi wa Ililika na kupelekea mnada na mgawo wa mifuko ya mawe yenye viambata vya dhahabu kusitishwa kwa kile kinachodaiwa mifuko ya serikali ilikuwa inanunuliwa kwa bei ndogo.

“Mgawo ulichelewa kwa sababu stahiki za serikali, zilikuwa haziwezi kupata fedha kama inavyotakiwa, kwani serikali imekuwa na stahiki zake lakini inaona ni vyema kuziuza kwa watu wengine ili wajipatie kipato.

“Sasa ilitokea sintohamu kwa wanunuzi kushuha bei kwa zile stahiki za serikali, na hatimaye kupelekea serikali kusitisha, sasa katika kusitisha, kuna maumivu, ambayo yamewathiri wachimbaji wetu” amesema.

Amesema Gerema amekutana na maofisa wa madini, usalama wa taifa, uongozi wa jeshi la polisi na halmashauri ya wilaya ya Geita na wameafikiana mgawo utaanza Jumatatu, Machi 03, 2025.

“Wapo watu wachache ambao wanatafuta kwa njia tofauti, ukienda mgodini kuna mwingine anafanya kazi ya kufundisha tu, yeye hataki kuchimba, mwingine yeye kazi yake ni kutembeza ulimi hivo ndivyo anavyoishi.

“Hatutakubalia watu wa aina hii watuharibie, dawa ni kumdhibiti tu mtu wa aina hiyo tunampiga sunspesion, ili watu wengine waweze kuendelea na shughuli zao”.

Katibu wa mgodi wa Ililirika, Veronica Fabian amekiri kuwa chanzo cha mgogooro ni baada ya baadhi ya wanunuzi kufanya hujuma mnadani kwa kununua mawe ya serikali kwa bei ndogo na mgodi ulifungwa kwa wiki mbili.

Amesema lengo la kusitisha mgawo wa mifuko ya mawe ya dhahabu ni kusimamia sheria, taratibu na kanuni kwa wachimbaji wadogo ili kuhakikisha kila mtu anapata haki yake ikiwemo ulipaji sahihi wa stahiki za serikali.

Mkaguzi Mkuu wa Mgodi, Kazimiri Faustine amesema mbali na mgogoro huo wa kimaslahi, wamesimamia kuhakikisha hakuna mtu mmoja ama kundi la watu linachafua usalama wa mgodi kwa kuanzisha machafuko.

Mchimbaji mdogo mgodini hapo, Tito Magumba amekiri kusitishwa kwa mgawo wa mawe ya dhahabu kwa muda wa wiki mbili imewaathiri hasa zaidi watu wa chini ambao ni vijana wanaozama shimoni kuchimba madini.

Naye Augustine Thomas amepongeza hatua ya Gerema kutoa suluhu ya mgogoro huo wa kimaslahi na kurejesha mgawo wa mawe ya dhahabu kwani itawapa molari ya kazi na kuwezesha vijana wa chini kupata stahiki zao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button