Geseco kinara wa mtihani wa ‘mock’ kanda ya ziwa

SHULE ya Sekondari Geita (GESECO) imeshika nafasi ya kwanza kwa upande wa Shule za Serikali katika matokeo ya Mtihani wa Utamilfu ( Mock) kidato cha nne 2025 Kanda ya Ziwa.
Mtihani wa MOCK kidato cha nne kanda ya ziwa ulijumuisha mikoa sita ambayo ni Geita, Kagera, Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyaga na ulifanyika kuanzia Julai 14, 2025 na kumalizika Agosti 01, 2025.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita Dk. Elfas Msenya ametangaza matokeo hayo Agosti 16, 2025 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu mjini Geita.
Amesema mtihani huo ulihusisha shule 1,401 kati yake shule 1,115 za Serikali na shule binafsi 246 kutoka halmashauri zote 43 pamoja na watahiniwa 151,649, wakiwemo wavulana 74,142 na wasichana 74,424.

Dk Msenya amemtaja mwanafunzi Alex Theojenes James wa Shule ya Sekondari Geita ndiye aliyeongoza kwa kupata ufaulu wenye ubora kwa kupata Divisheni 1.7
Aidha ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza umeongoza katika matokeo ya jumla ya Mtihani wa Utamilifu (MOCK) kwa kidato cha nne kanda ya ziwa mwaka 2025 baada ya kupata ufaulu wa jumla wa asilimia 94.11 kwa shule zote.
“Simiyu imeshika nafasi ya pili kwa asilimia 91.31, nafasi ya tatu ni Shinyanga kwa asilimia 89.71, Kagera nafasi ya nne asilimia 84.35, Geita nafasi ya tano asilimia 83.58 na Mara nafasi ya sita asilimia 80.58”, ameongeza Dk Msenya.
Dk Msenya ameagiza tathimini ya ifanyike kwa kina kwa ngazi zote ambazo ni mkoa, halmashauri na shule na mapungufu yatakayobainika masahihisho yafanyike kati ya Agosti 15 hadi 25, 2025.

Awali Mwenyekiti wa Maofisa Elimu Tanzania, Martin Nkwabi amesema kuwa ni watahiniwa 145,318 pekee kati yao wavulana 70,894 na wasichana 74,424 sawa na asilimia 95,83 walifanya mtihani.
“Watahiniwa 6,331 kati yao wavulana wakiwa 3,248 na wasichana 3,083 sawa na asilimia 4,17 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali hasa zaidi ikiwa ni utoro”, amesema Nkwambi.
Ifahamike kuwa Mkoa wa Geita umefanikiwa kutoa wanafunzi watatu walioingia kumi bora kutoka katika Shule ya Sekondari Geita na shule ya Wasichana Nyankumbu.



