GGML, OSHA zaokoa wachimbaji wanawake Geita

KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu ya Geita (GGML) imeungana na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kuimarisha usalama wa mazingira ya wachimbaji wadogo wanawake Mkoa wa Geita.

Mpango huo unajumuisha utoaji wa elimu ya uchimbaji salama pamoja na ugawaji wa vifaa kinga vyenye thamani ya sh milioni 24 kwa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Wanawake Mkoa wa Geita (GEWOMA).

Meneja Mwandamizi wa GGML kitengo cha Uendelezaji, Gilbert Mworia amesema hayo katika semina maalum kwa wachimbaji wanawake Mkoa wa Geita na kueleza mpango huo umeanza kwa kutoa mafunzo ya usalama mahala pa kazi kwa kushirikiana na OSHA pamoja na Ofisi ya Madini.

“Sisi kama kampuni ni jukumu letu kuhakikisha kwamba tunasaidia wachimbaji wadogo kwa sababu katika maeneo yetu ambayo tunafanya kazi tumezungukwa na wachimbaji wadogo.

“Vilevile sisi kama kampuni tumetoa vifaa vya kujikinga mahala pa kazi (PPE) kwa wanawake wote wa GEWOMA, tumetoa PPE kwa watu 50 kwa ajili ya kuweza kuwasaidia katika shughuli za uchimbaji”, amesema Mworia.

Meneja Mwandamizi wa GGML Idara ya Afya, Usalama, Mazingira na mafunzo, Dk Kiva Mvungi amesema maeneo ya wachimbaji wadogo yanahitaji tahadhari kubwa kutokana na muingiliano mkubwa wa watu.

Amesema elimu inayotolewa inalenga kuwaepusha wanawake na athari za kiafya ikiwemo Kifua Kikuu (TB) kutokana na tabia hatarishi za watu tofauti na ufanyaji kazi kwa mazoea, pasipo tahadhari.

Ofisa Mkaguzi Mwandamizi kutoka OSHA, Amina Nangu amesema sekta ya uchimbaji wa madini ina vihatarishi vingi na vyenye athari kubwa endapo kanuni za afya na usalama mahala pa kazi hazitozingatiwa.

Amesema endapo wachimbaji wadogo wakizingatia kanuni hizo itawasaidia kufanya kazi katika mazingira salama, kulinda afya zao na kuepuka ulemavu, magonjwa na uwekezaji usio na tija.

Naye Katibu wa GEWOMA, Makrina Fabian amekiri shirikisho hilo lina jumla ya wanachama 280 kutoka maeneo tofauti ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi bila elimu sahihi na vifaa kinga thabiti.

“Tunashukuru sana GGML kwa kutuletea vifaa kwa ajili ya kutulinda sisi kiafya, kwa sababu kabla ya kutupa hivi vifaa tulikuwa tunapata changamoto nyingi sana kujikinga na wadudu na kemikali,”amesema Makrina..

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button