GGML yaendeleza mapambano dhidi ya rushwa Geita

GEITA: KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu ya Geita (GGML) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo, itaandaa warsha ya siku mbili inayolenga mapambano dhidi ya rushwa na utoaji hongo.
Warsha hiyo itakayofanyika kuanzia Mei 13 hadi 14, 2025 katika kumbi wa Mtakatifu Aloysius mjini Geita.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa dhamira ya muda mrefu ya GGML kuendeleza maadili, uwazi na utawala bora katika jamii zinazozunguka maeneo ya shughuli zake.
Kampeni hiyo ya 2025 inakuja na mtazamo mpana zaidi unaojumuisha siyo tu warsha , bali pia mikutano ya kijiji 28 na kipindi maalumu cha redio cha saa moja, vyote vikiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa elimu ya kupinga rushwa kwa wananchi wengi zaidi.
Warsha hiyo ya siku mbili itawakutanisha washiriki kutoka taasisi za umma na binafsi kushiriki katika mijadala ya vitendo na mafunzo kuhusu maadili, mifumo ya kisheria, na njia za uwajibikaji katika jamii.
Mikutano ya kijijini itawawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika vita dhidi ya rushwa kwa kutoa maoni na kuuliza maswali.
“Rushwa inazuia maendeleo na kupunguza imani ya wananchi kwa taasisi,” alisema David Nzaligo, Wakili Mwandamizi wa GGML.
“Kupitia ushirikiano wetu na TAKUKURU pamoja na upanuzi wa mpango huu hadi ngazi ya vijiji, tunalenga kuwawezesha wananchi kupata maarifa na kujiamini katika kudumisha uwazi katika maisha yao ya kila siku.”
Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Geita imekuwa mshirika wa kimkakati katika kupanga na kutekeleza kampeni hii. Kamati ya pamoja ya wafanyakazi wa GGML na maafisa wa TAKUKURU inasimamia utekelezaji wa shughuli zote.
TAKUKURU inaendelea kutoa mwongozo wa kitaalamu na msaada ili kuhakikisha warsha hizo zinaendana na mazingira ya mikoa na kuwa na matokeo chanya.
Mpango huu unaakisi imani ya GGML kwamba mazingira yasiyo na rushwa ni msingi wa maendeleo endelevu. Huu ni mwendelezo wa kampeni na warsha mbalimbali zilizofanyika kwa miaka kadhaa huko Geita kwa lengo la kuimarisha utamaduni wa uadilifu katika taasisi na jamii kwa ujumla.