Gharama za kodi ziwe rafiki -Samia

PWANI: RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza Kongani ya Viwanda Kwala mkoani Pwani kuhakikisha gharama za kodi kwa wawekezaji zinakuwa rafiki ili kuweza kuvutia zaidi wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na gharama kuwa juu na hivyo kuwa kikwazo kwa wawekezaji wengi.
Rais Samia amebainisha hayo leo Julai 31, 2025 wakati akizindua Kituo cha Kimataifa cha Usafirishaji cha Kwala mkoani Pwani, baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye Kongani ya viwanda Kwala pamoja na uzinduzi wa safari za treni za mizigo za SGR.
Ameagiza pia kufuatwa kwa sheria zote za Tanzania ikiwemo ruhusa za uwekezaji na viwango vya bidhaa zinazozalishwa na wawekezaji nchini kama sehemu ya kuendelea kuweka heshima na sifa njema ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Niwaombe sana kuangalia na kufuata sheria zote za uzalishaji Tanzania. Ruhusa za uzalishaji lakini pia viwango vya bidhaa zinazozalishwa. Bidhaa zile zitatumika ndani ya nchi na kuna sehemu itakayokwenda nje. Zote zinazotumika ndani na zitakazotumika nje ziwe za viwango, hatutaki Tanzania ipeleke bidhaa za viwango hafifu kwenye masoko,” amesema Rais Samia.
Katika maelezo yake, Rais Samia Pia ameielekeza Wizara ya Uchukuzi na Taasisi zake zote zinazotoa huduma bandarini Dar es salaam kuhamishia huduma zote za Kibandari kuhamishia huduma zake kwenye Bandari Kavu ya Kwala kufikia Agosti 04, 2025 kama sehemu ya kuongeza ufanisi na uharaka katika kuhudumia mizigo, akisisitza umuhimu wa kasi, weledi na huduma bora za kwa Wateja mbalimbali.
Aidha, Rais Samia ameagiza malori yasiyokuwa na ulazima wa kuingia Jijini Dar es salaam kutofanya hivyo, akitaka yaishie Kwala mkoani Pwani kama sehemu ya kuondokana na changamoto ya msururu wa malori Jijini Dar es salaam, akiagiza pia Mkoa wa Pwani na sekta binafsi kutenga maeneo kwaajili ya utoaji wa huduma mbalimbali zitakazotokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi katika eneo hilo, akimuagiza pia Mkuu wa Polisi Tanzania kufungua kituo cha Polisi eneo hilo kama sehemu ya kuongeza ulinzi na usalama katika eneo hilo la kiuwekezaji.



