Ghasia : Kairuki ni lulu ya wanakibamba

DAR-ES-SALAAM : MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Hawa Ghasia, amesema mgombea ubunge wa Jimbo la Kibamba kupitia CCM, Angellah Kairuki, ni lulu ambayo wananchi wa jimbo hilo hawapaswi kuipoteza kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusimamia, kufuatilia na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Goba, jijini Dar es Salaam, Ghasia alisema Kairuki ana uzoefu mkubwa wa uongozi na anajua vyema namna ya kuisimamia Ilani ya CCM. “Kairuki haendi kujifunza ubunge. Amekuwa mbunge mara kadhaa, anaufahamu vizuri mfumo wa Bunge na Serikali. Ni mfuatiliaji na mtendaji makini ambaye anapewa jambo analikamilisha kwa ufanisi,” alisema Ghasia.

Amesema Kairuki amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo uwaziri na ujumbe wa Kamati ya Haki za Binadamu inayowakilisha Afrika katika Bunge la Dunia, hivyo ana uzoefu mpana na sifa za kuwatumikia wananchi wa Kibamba. “Wanakibamba msiipoteze lulu mliyopata. Angellah ni kiongozi anayejua kufuatilia bajeti na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati. Anaunganisha, hafanyi kelele, bali anafanya kazi,” alisema.

Aidha, Ghasia alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa wananchi wa Kibamba kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani. “Tunaomba kura kwa mafiga matatu Rais, Mbunge na Diwani. Kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa miaka minne imejidhihirisha katika elimu, afya, maji na miundombinu. Ni heshima kumpa kura za ushindi mkubwa,” alisema.

Amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, ada za shule kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari zimeondolewa, mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya kati na vyuo vikuu imeboreshwa, na miradi mikubwa ya kitaifa imeendelea kutekelezwa kwa ufanisi. “Hakuna mradi uliosimama. Bwawa la Nyerere linaendelea, SGR inajengwa, shule na hospitali zimeongezeka haya yote ni matokeo ya uongozi makini wa Dk. Samia,” alisisitiza.

SOMA: Kairuki aahidi kujenga barabara tisa Goba

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Goba, Laurence Mlaki, aliwaomba wananchi wa kata hiyo kumpa kura ili aweze kushirikiana na Kairuki kutatua changamoto za eneo hilo. “Ninaomba kura kwa Rais Dk. Samia, kwa Mbunge Angellah Kairuki na kwa mimi Diwani wenu. Miradi ya kimkakati imetekelezwa, uchumi umekua kwa zaidi ya asilimia 4.5, tuna SGR na Bwawa la Nyerere hivyo ni wakati wa kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na serikali yetu,” alisema Mlaki.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button