‘Hakikisheni watoto wanapata chakula shuleni’
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi Mohamed Ramadhan, amewaagiza maofisa elimu kuelekeza nguvu kuhakikisha watoto wanapata chakula wanapokuwa shuleni.
Ameyasema hayo katika kikao cha kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya hiyo eneo la Hospitali ya Wilaya ya Nsimbo, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya mkataba wa kwenda kusimamia afua za lishe.
“Maofisa elimu mpo hapa, naomba mtusaidie kwenye sekta zenu kuhakikisha kwamba kila shule ni lazima, sio ombi ila ni lazima mtoto apate chakula, ile bajeti yake ambayo angekula akiwa nyumbani basi ipelekwe shuleni, naomba hili tukalisimamie tena kikamilifu tena hili mkawashirikishe watendaji wa vijiji na kata pamoja na maofisa Elimu Kata,” amesema.

Pia ameagiza idara ya Kilimo na Mifugo kusisitiza uzalishaji wa makundi yote ya chakula, ili wananchi waweze kuzalisha virutubisho vinavyotakiwa kuliwa wakiwa nyumbani.
“Niombe bajeti zetu, na mikakati yetu katika utendaji wa idara zetu ujikite kuhakikisha kwamba virutubisho vyote vinapatikana, na moja ya virutubisho ambavyo tunavikosa kwa Mkoa huu ni matunda,” amesema na kuongeza:
“Bado tuna idadi chache ya aina za matunda kwenye eneo letu, na miche mbalimbali ya matunda kwenye ardhi yetu inakubali, hivyo tukaweke mkakati kabisa wa kutosha kwenda kupanda miti ya matunda”
Akitoa taarifa ya lishe kwa robo ya pili ya Oktoba hadi Desemba 2022, Ofisa Lishe Wilaya ya Nsimbo, Nickson Yohans, amesema changamoto ya uhaba wa vifaa tiba umesababisha kushindwa kupima hali ya udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano.
Amesema changamoto nyingine ni uhaba wa vyakula dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya, pamoja na uwepo wa idadi ndogo ya wanafunzi wanaopata chakula cha mchana licha ya shule nyingi kutoa chakula hicho kwa makundi maalum na wale waliopo katika mitihani.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Yohans amesema katika mwaka ujao wa fedha wametenga jumla ya Sh milioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe kutoka katika mapato ya ndani.
Akifunga kikao Mwenyekiti wa kikao hicho Dk. Wambura Waryoba, ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe, amesema kupitia mikutano ya vijiji, mratibu pamoja na Mganga Mkuu wa Wilaya wanapaswa kwenda kutoa elimu ya lishe kwa wazazi.
Amesema kupitia elimu hiyo itakayotolewa, wazazi wafahamu kuwa uelewa na ufaulu wa watoto wao ni pamoja na mchango wao katika maeneo ya lishe licha ya baadhi ya wazazi kulalamika kuwa wanapitia kipindi kigumu kinachofanya baadhi ya kaya kula mlo mmoja kwa siku.
Ameshauri kuwa katika kipindi cha mavuno ni vyema wazazi wakawasiliana na walimu ili kujua bajeti ya mtoto awapo shuleni ni kiasi gani na kutengeneza utaratibu wa chakula kutunzwa mashuleni.



