Hati yakwamisha kesi ya ‘madada poa’

DAR ES SALAAM; KESI ya kufanya vitendo visivyo vya heshima kwenye sehemu za umma inayomkabili Amina
Ramadhani na wenzake 17, imeshindwa kuendelea kusikilizwa hoja za awali kwa sababu hati ya mashtaka ilipelekwa kwa msajili.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Aisha Iddi, Mariana Sia, Mwajuma Hamza, Mariamu Hassan,
Najma Hamisi, Sabrina Gabriel, Mariam Kitamoga, Elizabeth Michael.

Wengine ni Rosemary John, Recho Kindole, Lobi Daudi, Diana David, Jackline Daniel, Mwajuma Bakari, Jenifa John, Zainabu Hamisi na Recho Bakari.

Advertisement

Katika kesi hiyo, ilidaiwa Juni 14, 2024 katika maeneo ya Sinza Mori, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam washtakiwa wote 18 walikutwa na tuhuma ya kujiweka katika namna ambayo sio sawa mbele za umma na kufanya vitendo visivyofaa na kuvaa mavazi yasiyokubalika kwa nia ya kufanya ukahaba.

Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi, Janeth Mgaya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Sokoine Drive (Jiji) ambaye alijitoa katika kesi hiyo.

Awali Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi aliwaita majina washtakiwa na kukuta washtakiwa wawili ambao
ni mshtakiwa namba mbili na 17 hawakuwepo mahakamani na kuiomba mahakama itoe hati ya ukamataji ili
waweze kukamatwa.

Mawakili wa utetezi, Peter Madeleka, Jebra Kambona na Maria Mushi walidai kuwa bado haijajulikana kesi hiyo imepangwa kwa hakimu gani na kuiomba mahakama isizingatie ombi la upande wa mashtaka kwa sababu haijajulikana kuwa hakimu huyo ndio aliyepangwa kusikiliza kesi hiyo au sio.

“Pia tungefuatilia mahudhurio ya washtakiwa ambao hawapo mahakamani na tupewe nafasi ya kujiridhisha
kuwa kama wana tabia ya kutofika mahakamani au ni leo tu,” alisema Kambona.

Wakili Mbilingi alidai kuwa anahofia kuwa washtakiwa hao wanaweza kukimbia kama mshtakiwa
mmoja wa kwenye kesi inayomkabili Mariam Yusuph na wenzake ndio maana aliomba hati ya ukamataji ili waweze kuwakamata.

Hakimu Kasebele alisema kuwa hati ya mashtaka imepelekwa kwa msajili na pia hakuweza kusema chochote
kwa wakati ule kwa sababu kesi hiyo haijajulikana itasikilizwa na hakimu gani.

Aliongeza kuwa tarehe ijayo itajulikana kuwa kesi hiyo imepangwa kwa hakimu gani ambaye ataendelea kuisikiliza.

Pia alitoa onyo kwa washtakiwa kuwa wanatakiwa kufika mahakamani na kama wasipofika watafutiwa
dhamana zao na hawatapata dhamana tena.

Vilevile aliutaka upande wa mashtaka kufuata na kuzingatia amri ya mahakama
kama inavyoelekeza ili haki iweze kutendeka. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 4, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.