MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillius Wambura amesema jeshi hilo halitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya wahalifu.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza wakati wa hafla ya kuwavisha nishani maofisa wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali, hafla iliyofanyika uwanja wa Polisi Mabatini.
Amesema Jeshi la Polisi nchini limedhamiria kuhakikisha amani inatawala na kusisitiza kuwa uhalifu na wahalifu havina nafasi Tanzania.
“Hatutarudi nyuma na kuacha wahalifu wanatamba ndani ya nchi yetu,” amesisitiza IGP Wambura na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuthamini kazi nzuri zinazofanywa na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali za kulinda raia na mali zao.
“Rais Samia ameandika alama kwenye mioyo yetu kwa waliotunukiwa na wengine, ni alama ambayo inaendelea kukaa ndani ya mioyo yetu kwa muda mrefu sana,” amesema Wambura.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo nchini.