Huu ndio Utanzania halisi

KILA taifa hujipambanua kwa utamaduni na hulka ya watu wake kama utambulisho wake duniani. Yapo mataifa ambayo hutambulika kwa nidhamu, uadilifu, bidii katika kazi, uaminifu, usawa na usiri.

Vivyo hivyo, Tanzania inajitambulisha kwa amani, upendo na utu vinavyoakisiwa katika maisha ya kila siku ya wananchi wake.

Mantiki ya kujipambanua hivyo ni kulinda utambulisho wa kitaifa, kukuza umoja na kuonesha thamani zinazowaongoza katika dunia yenye tamaduni na mitazamo tofauti.

Kwamba, Tanzania ni taifa linalojitambua, lenye watu wanaothamini amani, maelewano na utu kuliko tofauti zao za kisiasa, kidini au kikabila.

Tumeiona sura hii ya kweli ya Utanzania kupitia matamko, misimamo na hatua za Watanzania baada ya sintofahamu iliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu.

Badala ya kuchochea zaidi migawanyiko, sauti za Watanzania wa kada tofauti zimeonesha busara, uzalendo na umoja wa kweli kwa kuhimiza maridhiano, mazungumzo na kujisahihisha.

Mathalani, waliokuwa wagombea wa urais kupitia vyama vya upinzani wameonesha ukomavu wa kisiasa na uzalendo wa hali ya juu kwa kutaka falsafa ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya (4R) itekelezwe na vyama vyote bila ubaguzi.

Hatua hii ni ushahidi kwamba wanasiasa hawa hawasukumwi na madaraka pekee, bali pia wana dhamira ya kuona taifa linaendelea kuwa moja, lenye haki na amani. Wanadhihirisha ukweli kwamba upinzani wa kweli ni ule unaojenga na si kubomoa.

Kwa upande mwingine, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limewaomba wananchi kusimama pamoja kama taifa, kuzungumza na kujisahihisha ili vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu zisitokee tena.

Wanataaluma hawa kutoka vyombo tofauti vya habari vyenye sera tofauti, pia wamedhihirisha ambavyo linapokuja suala linalohusu amani na utulivu, Watanzania husimamia utamaduni wa hulka yao ya kuhimiza umoja, amani, utulivu, kuzungumza na kujisahihisha.

Jukwaa limeonesha kwamba vyombo vya habari ni chachu ya umoja na si chanzo cha mgawanyiko.

Aidha, kauli yake ni mwendelezo wa utamaduni wa mazungumzo uliojengeka tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliamini mazungumzo ni nguzo ya amani.

Vilevile, katika kile ambacho tunaona Utanzania halisi unaendelea kudhihirika, ni hatua ya wananchi wa kawaida pia kuonesha uelewa mkubwa wa masuala ya kitaifa kwa kuonya na kukemea matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, hasa maudhui yanayochochea chuki na vurugu.

Hii ndiyo hulka ya Watanzania na Tanzania yenye busara, subira na heshima kwa utu wa mtu mwingine. Ni Watanzania hawa wanaoamini kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuvuruga undugu na upendo uliotukuka.

Sifa kuu za Utanzania ni umoja, upendo, uvumilivu, heshima na uadilifu ambao ni nguzo muhimu zinazofanya nchi iwe kisiwa cha amani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button