Igumbilo kumpa zawadi ya kiwanja Ngajilo ili awe jirani na changamoto zao

Wakati siku za kuelekea uchaguzi mkuu zikihesabika, wakazi wa Kata ya Igumbilo, Manispaa ya Iringa, wametoa ahadi ya kipekee kwa mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, wakimuahidi kumpa eneo kwa ajili ya kujenga makazi yake ndani ya kata hiyo.
Ahadi hiyo imekuja ikiwa ni zawadi ya kwanza kwa Ngajilo kutoka kwa wananchi tangu aanze kampeni zake katika kata zote za jimbo hilo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Ulonge, mgombea udiwani wa kata hiyo Jackson Chatanda alisema wananchi wa Igumbilo wamemuahidi kumpa eneo hilo ili kumfanya Ngajilo awe karibu zaidi na changamoto zao za kila siku.
“Tumeamua kuweka ahadi ya eneo hapa Igumbilo ili awe jirani nasi. Akiwa mkazi wa hapa, atazitambua kwa ukaribu zaidi changamoto zetu na kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka,” alisema Chatanda.
Akitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili kata hiyo, Chatanda alisema ni pamoja na ubovu wa barabara, upungufu wa miundombinu ya elimu na huduma duni za afya.
Kwa upande wake, Ngajilo alisema ameguswa na hatua hiyo ya wananchi wa Igumbilo na kuahidi kuwa hatowaangusha endapo atapata ridhaa ya kuwaongoza kama mbunge.
“Igumbilo ni kata ya kwanza kunipa zawadi kabla hata sijachaguliwa. Hii ni heshima kubwa, na ninawahakikishia sitawaangusha,” alisema Ngajilo huku akipigiwa makofi.
Aliongeza kuwa kutokana na jiografia ya Igumbilo iliyo pembezoni mwa manispaa, ni lazima juhudi zielekezwe katika kuboresha huduma za kijamii kama afya, maji, barabara na umeme.
“Tunajua huduma nyingi zinapatikana mjini, lakini lazima tuzilete huku. Tutahakikisha kituo cha afya cha Igumbilo kinakuwa na huduma zote muhimu ikiwemo ambulance ya kubeba wagonjwa,” alisema.
Ngajilo pia aliahidi kushirikiana na mashirika ya huduma za maji (IRUWASA) na umeme (TANESCO) kuhakikisha vijiji kama Matungulu vinapata huduma hizo haraka.
Akizungumzia maendeleo ya makazi, alisema serikali itahakikisha wananchi wanapimiwa ardhi zao na kupatiwa hati miliki ili kuongeza usalama wa mali zao.
Aidha, aliahidi kusimamia ujenzi wa soko la kisasa la Igumbilo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, pamoja na kuwawezesha vijana na akinamama kupitia mikopo ya vifaa vya uzalishaji kama mashine za kutengeneza juisi na kufyatua tofali.
“Tukianza kuwawezesha wananchi kujiajiri, tutakuwa tunawaondoa kwenye umasikini hatua kwa hatua. Pia michezo tutaiwekea nguvu — ni ajira, ni fedha,” alisema Ngajilo.