Ilani NCCR-Mageuzi, ACT Wazalendo, AAFP na ajenda ya kukuza uchumi

KAMPENI za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025 zinaendelea kwa kasi kwa vyama kunadi sera na ilani zao kwa kila kimoja na mgombea wake kikitaka kichaguliwe. Hivi karibuni chama cha Allience for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) nacho kimezindua Ilani yake kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 yenye vipaumbele saba.

Moja ya vipaumbele vilivyoainishwa kwenye ilani hiyo ni kuwa, kama kitachaguliwa na kushika dola, ACT-Wazalendo inakusudia kujenga uchumi wa watu unaojitegemea na kuzalisha ajira milioni 12. Kupitia ilani hiyo ACT- Wazalendo inasema ikichaguliwa, serikali yake itatengeneza ajira mpya milioni 2.8 zitakazotokana na viwanda vinavyotumia malighafi za ndani kwa asilimia 85 katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

Mbali na ACT-Wazalendo, vyama vya National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi) na Chama cha Wakulima (AAFP) navyo katika ilani zao vinasema vinakusudia kuinua na kuimarisha uchumi katika namna mbalimbali kuchochea kasi ya maendeleo ya taifa.

ACT-Wazalendo

ACT-Wazalendo katika Ilani ya Uchaguzi ya 2025/2030 inaweka bayana dhamira yake kuifanya nchi kuwa na uchumi imara na endelevu. Inasema ili taifa liwe na uchumi imara na endelevu, lazima uchumi huo utokane na watu wenyewe kupitia shughuli zao mbalimbali kama kilimo, uvuvi, ufugaji, viwanda, uvunaji wa rasilimali, utalii na biashara zikiwamo ndogondogo.

Kwa mujibu wa ilani hiyo, endapo kitachaguliwa na kuunda serikali, chini ya usimamizi wake, Serikali ya ACT-Wazalendo itakuza uchumi ili kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu ifikapo mwaka 2030. Kwamba kitafanya hivyo kikilenga kuhakikisha hakuna wananchi wanaoachwa katika umasikini na ufukara.

Chama hicho kinaahidi kuanzisha maeneo maalumu ya viwanda na biashara yatakayoanzisha viwanda vikubwa vyenye uwezo wa kuajiri watu wasiopungua 20,000 katika kanda ili kuongeza ajira kwa vijana nchini kote.

Kinaahidi kutunga sheria itakayoweka utaratibu wa kuhakikisha asilimia 80 ya bidhaa na huduma zinazotumika kwenye miradi na shughuli za ujenzi na maendeleo za serikali zinatumia malighafi na bidhaa za ndani, hususani zinazotoka katika eneo husika ili kufungamanisha na mnyororo wa thamani. Ilani hiyo pia inaeleza kuwawekea maeneo maalumu wafanyabiashara wadogo (wamachinga) miundombinu wezeshi katika maeneo ya mijini ili waweze kufanya biashara zao katika mazingira bora.

Kupitia kilimo, ilani hiyo inasema ACT Wazalendo kinadhamiria kufanya mapinduzi ya kilimo na kuifanya sekta hiyo kukua kwa asilimia nane kwa mwaka na kuongeza mavuno maradufu zaidi kwa eneo la uzalishaji na kuhakikisha kilimo kinabadili maisha kwa kuwekeza asilimia 20 ya bajeti ya maendeleo kwenye sekta ya kilimo.

Aidha, serikali itakayoundwa na chama hiyo endapo kitapewa ridhaa na wananchi kuongoza, itafungamanisha sekta ya kilimo na sekta ya viwanda, ili kuhakikisha asilimia 85 ya malighafi ya viwanda vya ndani inatokana na wakulima wa ndani.

ACT-Wazalendo kupitia ilani hiyo inaahidi kupanua kilimo cha umwagiliaji hadi kufikia hekta milioni mbili ili kukuza kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi. Katika viwanda, chama hicho kinaahidi kupiga marufuku uuzaji wa malighafi nje ya nchi isipokuwa pale tu, ambapo uwezo wa ndani wa kuzalisha bidhaa za mwisho ni mdogo.

Kwamba, hatua hiyo inalenga kulinda ajira na kuongezea thamani rasilimali za nchi ndani ya nchi. Aidha, kinaahidi kutoa kipaumbele kwa viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwapunguzia gharama za uzalishaji.

Gharama hizo ni pamoja na zile za umeme, maji, kodi, huduma za usafirishaji na kutoa ruzuku kwa viwanda vinavyochipukia. Kama kitachaguliwa, chama hicho kinasema kinakusudia serikali yake kutengeneza ajira milioni moja kupitia zao la pamba kwa kufufua viwanda vya kuchakata pamba na kuzalisha nguo.

Chama cha AAFP

Ilani ya Chama cha Wakulima (AAFP) inasema chama kinakusudia kuwapa ujuzi wakulima katika utafiti, masoko, pembejeo, mbegu bora sambamba na kuweka maabara za kisasa katika kila kata. Aidha, ilani inakusudia kukuza uchumi wa kujitegemea. AAFP inataka kuwawezesha wananchi kuwa na kipato kisichopungua Sh 20,000 kwa siku. Chama hicho pia kinakusudia kuzalisha ajira milioni 15 kupitia mfumo rasmi na mfumo usio rasmi na kuweka masharti nafuu kwa wawekezaji wazawa na wale wa kigeni.

Kinaahidi kuweka mpango kwa vijana wote waliomaliza vyuo vya kati na vyuo vikuu katika ajira rasmi na zisizo rasmi kwa ajili ya uzalishaji mali. Inaeleza kuwa chama hicho kitatumia na kusimamia rasilimali za nchi kama vyanzo endelevu vya mapato katika kukuza uchumi wa kujitegemea.

Aidha, kitasimamia kuongezwa kwa vyanzo vingine vya mapato kadiri ya mazingira ya fursa zinazozunguka maeneo. Kwa mujibu wa ilani hiyo, pia serikali katika awamu ya kwanza ya uongozi wa chama hicho endapo kitachaguliwa itaweka mpango wa maendeleo na kipaumbele chake kitakuwa uzalishaji bora katika bidhaa za kilimo, ufugaji na uvuvi.

NCCR Mageuzi

NCCR-Mageuzi nacho kinaahidi kuhamasisha wananchi na kuwawezesha kufanya ujasiriamali katika viwanda kwa kubuni na kujenga viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali.SOMA: Wakulima kuwezeshwa na NCCR-Mageuzi

Inaeleza mkakati huo utatekelezwa kwa kuendeleza viwanda vidogo na vya kati hasa vile vinavyosindika mazao. Chama hicho pia kinatoa ahadi ya kuhakikisha malighafi zote za Tanzania zinasindikwa kabla ya kusafirishwa nje ya nchi na kuanzisha viwanda vya msingi vinavyotumia malighafi ya chuma katika eneo la Liganga na Mchuchuma. Kinaahidi kujenga uchumi imara kwa kutekeleza ahadi ya kudhibiti mfumuko wa bei ili ubaki katika tarakimu moja.

NCCR-Mageuzi pia inaahidi kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni kwa kuepuka kuagiza bidhaa zisizo za lazima kutoka nje. Ahadi nyingine ya NCCR-Mageuzi ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato na kupanua wigo wa walipakodi.

Katika kilimo NCCR-Mageuzi inaamini kuwa asilimia 87 ya nguvukazi imejikita kwenye kilimo na ufugaji na kwa kuwa asilimia 44 ya pato la taifa inatokana na sekta hiyo, chama hicho kinaahidi kuwezesha wakulima kwa zana bora za kisasa ili kuongeza tija na uzalishaji kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuboresha mifumo ya utoaji wa ruzuku.

Chama hicho kinasema kikiingia madarakani, serikali yake itawezesha wananchi katika miradi ya uzalishaji wa bidhaa kwenye viwanda vya kusindika kwa ajili ya masoko ya nje ya nchi kwa kutumia malighafi zinazotokana na kilimo. Sambamba na hilo NCCR-Mageuzi inaahidi kuhamasisha vijana kuunda vikundi vya ujasiriamali ili kuweka mazingira bora ya kupata mikopo yenye riba nafuu na masharti nafuu.

Habari Zifananazo

6 Comments

    1. JOIN US Everybody can earn 250/h Dollar + daily 1K… You can earn from 6000-12700 Dollar a month or even more if you work as a part time job…It’s easy, just follow instructions on this page, read it carefully from start to finish… It’s a flexible job but a good earning opportunity. tab for more detail thank you……..
      .
      This is my main concern……………………………………. http://Www.Cash43.Com

    2. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
      .
      M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→→→→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button