INEC yawapa somo wasimamizi Shinyanga, Simiyu

SHINYANGA; WASIMAMIZI wa uchaguzi 83 kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu wametakiwa kusimamia viapo vyao na kujitoa kwenye chama chochote cha kisiasa kwenye kipindi hiki cha uchaguzi ili kuepuka migogoro.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ( INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Jacobs Mwambegele amesema leo wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya siku tatu kwa waratibu,wasimamizi na wasimamizi Wasaidizi .
Jaji Mwambegele amewaomba wasimamie viapo vyao vya kutunza siri na kutokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa katika kipindi chote cha uchaguzi na kutekeleza vizuri majukumu yao.
“Tume iliwaridhia maofisa uchaguzi na maofisa ununuzi kutekeleza kazi za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo uteuzi wenu umezingatia masharti ya kifungu cha sita(1),(2) na 5 na kifungu cha nane ( 1) na( 2) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani,”amesema Mwambegele.

Amewasihi wajiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi, pia wahakikishe wanazingatia ipasavyo katiba ,shera, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na tume.
Jaji Mwambegele amesema vyama vyote vya siasa vilivyo na usajili vishirikishwe kwa ukamilifu kwa hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya katiba, sheria,kanuni na maelekezo.

Jaji Mwambegele amesema ajira za watendaji wa vituo zizingatie kuajiri watendaji wenye weledi wanaojitambua, wazalendo, waadilifu na wachapakazi na kuacha upendeleo kwa kuajiri ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.



