Iringa waenda Geita kujifunza sekta ya madini

GEITA; JUMUIYA ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Iringa imefanya ziara ya mafunzo wilayani Geita kwa ajili ya kupata uelewa wa mifumo sahihi ya kuongeza mapato katika halmashauri kupitia sekta mbalimbali.

Ziara hiyo ililenga kuwajengea uwezo viongozi wa ALAT Iringa namna ya kutunga na kusimamia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya ukusanyaji wa mapato husani kwenye sekta ya madini.

Makamu Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Iringa na Makamu mwenyekiti Halmashauri ya Mafinga, Regnant Kivinge amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara hiyo.

Advertisement

Kivinge amesema Manispaa ya Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita zimepiga hatua kwenye kukusanya mapato katika sekta ya madini, ambayo inachangi takribani asilimia 75 ya mapato ya halmashauri hizo.

Amesema mafanikio hayo ni darasa kwa halmashauri za Mkoa wa Iringa na nchi nzima kwa ujumla na imechangiwa kwa kiasi kikubwa na usimamizi mzuri wa sheria ikiwemo Sheria ya Uwajibika wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Amesema elimu waliyopata itasaidia kuondoa utegemezi mkubwa wa mapato kutoka kwenye mazao ya misitu pekee na kuwekeza pia kwenye sekta ya madini kuanzia uchimbaji mdogo, uchimbaji wa kati na mkubwa.

“Kimsingi tumejifunza mengi, tumeona namna gani wanakusanya ushuru, kuanzia uchimbaji mdogo kule chini, lakini mnyororo mzima wa thamani mpaka madini yanafika sokoni.

Makamu Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Iringa, Regnant Kivinge

“Naamini na sisi tumejifunza tukirudi Iringa inaweza kutusaidia na sisi tunaamini kwenye halmashauri zetu tunaweza tukafanya vizuri,” amesema.

Mjumbe wa ALAT Taifa, Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Mfundi, Grace Mgina amekiri mfumo wa ukusanyaji tozo kwa wachimbaji wadogo Iringa haujawekwa sawa hivo wataufanyia mabadiliko.

Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Elias Ngole amesema muongozo mzuri wa tozo kuanzia uchimbaji, uchakataji, usafishaji, uchenjuaji mpaka biashara ya dhahabu ndio kiini cha mafanikio.