Jaji Mkuu atoa maagizo dhamana kesi za jinai
JAJI Mkuu wa Tanzania, George Masaju ameziagiza mahakama za hakimu mkazi, wilaya na mwanzo zitoe dhamana kwa washitakiwa kwa mashauri yote ya jinai yenye dhamana isipokuwa kama kuna sababu ya msingi.
Masaju alitoa agizo hilo Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria yakiwa na kaulimbiu “Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa”.
Ameagiza mtu anapoomba dhamana uamuzi wa kumpa au kumkatalia utolewe siku hiyo ya kuwasilisha ombi lake mahakamani.
“Hii inasaidia kupunguza mianya ya rushwa lakini pia inawezesha haki ya dhamana kupatikana mapema ipasavyo,” alisema Masaju.
SOMA: Jaji Mkuu awataka wahitimu wapya kudumisha haki
Alisema kwa makosa ambayo kisheria yanadhaminika mahakimu wanawajibika kuwajulisha watuhumiwa haki ya dhamana mara tu wanapofikishwa mbele yao.
“Hatua hii inawawezesha wananchi wanaotuhumiwa kwa makosa ya jinai kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii na kuhudhuria mahakamani wakitokea nyumbani hadi mashitaka dhidi yao yanapokuwa yametolewa hukumu/maamuzi mahakamani ipasavyo kwa mujibu wa Ibara 13(6)(b) ya Katiba,” alisema Masaju.
Alisema hatua kuhusiana na dhamana kwa washitakiwa/watuhumiwa zimepunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani na kuleta unafuu katika gharama za uendeshaji wa magereza.
Jaji Mkuu ameipongeza serikali kwa hatua za ujenzi wa mahakama za ngazi zote nchini.
“Hatua hii inachochea, kuongeza na kukuza mchango wa mahakama katika ustawi na maendeleo ya taifa kwa kuwa wananchi wenye migogoro wanaifikia mahakama kwa ukaribu na wanaokiuka Katiba na sheria kuwajibishwa mapema kwa mujibu wa ibara ya 26 ya Katiba,” alisema Masaju.
Dira ya Mahakama ni haki sawa kwa wote mapema ipasavyo na kwamba msingi wa dira hiyo ni Ibara ya 107A(1 (2)(a)(b) na ibara 107B ya Katiba ya Tanzania.
Masaju alisema Mahakama ya Tanzania inafanya ugatuzi wa Mahakama ya Rufani ili mahakama hiyo ya juu kabisa nchini iwepo katika baadhi ya kanda za mahakama nchini ambazo tayari zina Masjala Ndogo.
“Waheshimiwa majaji wa Mahakama ya Rufani, naibu wasajili na watumishi wote wa Mahakama ya Rufani watakaokuwa katika ofisi za kanda wataendelea kupata haki na stahili zao za utumishi ipasavyo kama ilivyo kwa
watumishi watakaokuwa makao mkuu Dodoma,” alisema.
Aliongeza: “Lengo la ugatuzi huu ni kusogeza tu huduma za mahakama karibu na wananchi ili kuwezesha haki kupatikana mapema ipasavyo”.
Masaju alisema katika ugatuzi huo baadhi ya majaji watafanya kazi wakiwa katika masjala za kanda kama Dar es Salaam ambayo itahudumia pia Zanzibar kabla ya kuanzishwa kwa masjala nyingine ya kudumu Zanzibar.
Kanda nyingine ni Arusha, Mwanza, Mbeya na Tabora.
“Tunachukua hatua ipasavyo kuifanya mahakama kuendelea kuwa mahali pa kupata haki mapema ipasavyo na si mahali pa kuegesha mashauri baina ya wadaawa kama ambavyo wadaawa wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakikwepa kuwajibika kimikataba na kisheria katika mashauri ya madai kwa aina zake zote,” alisema Masaju.



