Jaji Mkuu awataka wahitimu wapya kudumisha haki

DODOMA: JAJI Mkuu wa Tanzania, George Masaju, amewataka mawakili nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uaminifu na kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili ya taaluma ya uwakili.

Amesisitiza kuwa mawakili wanapaswa kuwa nguzo ya utawala wa sheria na si chanzo cha uvunjifu wa amani katika jamii.

Akizungumza katika mahafali ya 73 ya mawakili wapya 774 yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mabeyo, jijini Dodoma, Jaji Mkuu alisema mawakili wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha haki inatendeka bila upendeleo na bila kukiuka misingi ya sheria.

“Nachukua nafasi hii kuwaasa kwamba mnatakiwa na mtaendelea kuwa watu wenye fikra pevu kama mawakili. Ni lazima muwe makini na kuhakikisha haki inaonekana na kutendeka. Pia mnapaswa kuwa waadilifu na kuzingatia Katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Jaji Mkuu Masaju.

Katika mahafali hayo, mmoja wa wahitimu ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Georgina Matagi, ambaye ameungana na mawakili wapya 774 kuapishwa rasmi.

Akizungumza baada ya kutunukiwa sifa za uwakili, SSP Matagi alisema elimu aliyoipata itaongeza uwezo wake wa kulitumikia taifa na jamii inayomzunguka.

Amesema mafunzo ya uwakili yamemjengea uelewa mpana katika masuala ya sheria, hivyo ataitumia elimu hiyo kuimarisha huduma za kisheria na kusimamia haki kwa uadilifu katika majukumu yake ya kila siku.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button