Jesca aendelea kuwatumikia wananchi Iringa Mjini, kwa nguvu zote

Zikiwa zimebaki takribani wiki tatu kabla ya Agosti 3, Bunge litakapokuwa limevunjwa rasmi, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, ameendelea kuthibitisha kuwa utumishi wa umma si hadhi bali ni dhamira ya dhati kwa kuendeleza harakati za maendeleo.

Katika hatua ya hivi karibuni, Jesca ameshuhudia kukabidhiwa kwa eneo la kazi kwa ajili ya kuanza rasmi kwa Mradi mkubwa wa TACTICS—wa kubadilisha miji kwa njia ya ushindanishi, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya Sh bilioni 20.2.

Mradi huu wa kihistoria unatarajiwa kuchukua miezi 15 hadi kukamilika, chini ya utekelezaji wa mkandarasi mzawa, Dimetoclasa Real Hope Ltd, na unajumuisha miradi mikuu mitatu ambayo inalenga kuinua maisha ya wakazi wa Iringa Mjini kwa viwango vipya.

Miradi hiyo ni pamoja na
ujenzi wa soko la kisasa la Kihesa, ujenzi wa barabara ya kilomita 5.2 kutoka Mkimbizi hadi Mtwivila, na ujenzi wa jengo la ofisi ya wahandisi wa TARURA, Manispaa ya Iringa.

Akizungumza mbele ya viongozi wa serikali, wataalamu wa TARURA, madiwani wastaafu, na wananchi waliojitokeza kwa wingi, Jesca alisema miradi hiyo ni matunda ya uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuonesha upendo kwa Iringa kwa kuipatia fedha nyingi za miradi ya maendeleo.

“Hizi si fedha za mapato ya ndani ya Manispaa yetu. Ni fedha kutoka Serikali Kuu kupitia juhudi za Rais wetu mpendwa, Mama Samia. Ni wajibu wetu sasa kuuenzi mradi huu kwa kuulinda na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake,” alisema.

Katika miradi hiyo, ujenzi wa soko la Kihesa umeelezwa kuwa wa kimkakati, kwa kuwa ni eneo linalohudumia wakazi wengi wa Iringa Mjini, hususani wafanyabiashara wadogo.

Soko hilo litajengwa kwa viwango vya kisasa likiwa na miundombinu bora ya usafi, mifumo ya kukinga majanga, na mazingira rafiki ya biashara kwa wote, likilenga kukuza uchumi wa mtaa hadi mkoa.

Mbunge huyo alisisitiza pia umuhimu wa wananchi wa maeneo husika kupewa ajira za muda wakati wa utekelezaji wa mradi, ili waone faida ya moja kwa moja ya uwekezaji huo mkubwa katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Iringa, Mhandisi Barnaba Jabiry, alitumia nafasi hiyo kuishukuru ofisi ya mbunge kwa ushirikiano wake wa karibu tangu hatua za mwanzo za maandalizi ya mradi.

Alieleza kuwa ujenzi wa barabara ya Mkimbizi–Mtwivila utarahisisha huduma kwa jamii na kuwaunganisha wakazi wa maeneo hayo kwa ufanisi zaidi.

Madiwani wastaafu wa kata za Kihesa, Mkimbizi na Mtwivila walionyesha furaha yao, wakisema Jesca amekuwa mfano wa kuigwa kwa namna alivyojitoa kushirikiana nao hata baada ya muda wao wa uongozi kumalizika.

Walisisitiza kuwa mradi huu unakwenda kufungua fursa za kimaendeleo katika elimu, afya, biashara na usafirishaji.

Naye Injinia Mbulinyingi Nkumulwa kutoka kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Ltd, aliahidi kutekeleza kazi hiyo kwa viwango vya hali ya juu na kukamilisha kwa wakati.

Aliomba ushirikiano kutoka kwa wananchi na viongozi ili kufanikisha utekelezaji bora wa mradi.
Mradi wa TACTICS unatajwa kuwa moja ya miradi mikubwa kuwahi kutekelezwa Iringa Mjini kwa mkupuo mmoja, na ni sehemu ya ndoto ya muda mrefu ya kuibadilisha Iringa kuwa mji wa kisasa.

Kwa Mbunge Jesca Msambatavangu, huu ni uthibitisho kuwa utumishi wa kweli haupimwi kwa muda wa kubaki kazini, bali kwa kasi na uzito wa kazi hadi dakika ya mwisho, alisema mmoja wa wananchi wa kata ya Kihesa, Jackson Mbedule.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button