JK: Rais wa Namibia mfano wa kuigwa Afrika

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah ni kiongozi wa mfano Afrika.
Kikwete alisema hayo alipozungumza katika mhadhara wa kitaaluma ulioandaliwa na chuo hicho na kuhudhuriwa na Rais Nandi-Ndaitwah jana.
Alisema UDSM inajivunia kuwa chuo kinachotoa wataalamu bora na mashuhuri ambapo rais huyo ni mmoja wa watu hao ambao chuo inajivunia kuwa nao.
Kikwete alisema kwa kuwa kati ya marais wachache wanawake amesaidia kufungua njia kwa viongozi wa sasa na baadaye wanawake ambao watainuka na kuifanya jamii kuwa bora.
“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinajivunia kukuhesabu kuwa miongoni mwa wahitimu wake mashuhuri, kwa kutambua mchango wako mwaka 2020 nikiwa Mkuu wa chuo nilikutunuku Shahada ya Heshima na ni jambo ambalo ninajivunia. Heshima hiyo ilikuwa ni kutambua mchango wako wa kipekee katika utumishi wa umma, diplomasia na harakati za ukombozi,” alisema.
Kikwete alisema Tanzania na Namibia zina historia ndefu ya mshikamano iliyojengwa na harakati za uhuru, haki kwa jamii na uwepo wake chuoni hapo kwa mara nyingine unathibitisha dhamira ya pamoja ya kuendeleza ukaribu.
“Nilihudhuria hafla ya kuapishwa kwako, nilijisikia furaha sana, nikiwa nimekufahamu kwa miaka mingi wakati ukiwa hapa kama Mama SWAPO na tulipokuwa serikalini pamoja, ilikuwa ni hatua kubwa na ya kihistoria kwangu pia,” alisema.
Kikwete alisema wasilisho la kiongozo huyo jana lilitoa hamasa kwa wanawake wa rika zote kwamba wakiwa na malengo na wakayasimamia watafanikiwa kufikia ndoto zao.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye alisema historia ya Rais Netumbo inahusiana na urithi wa chuo hicho kikiwa ni kitovu cha fikra za kimapinduzi na taa ya kujenga Uafrika.
Profesa Anangisye alisema katika miaka ya 1970 na 1980 chuo hicho kilitoa hifadhi na msaada wa kimaarifa kwa ajili ya harakati za ukombozi kusini mwa Afrika na Wanamibia wengi waliopigania uhuru walipata maarifa ya kupigania uhuru na mshikamano hapo.
Makamu Mkuu wa UDSM Mipango, Fedha na Usimamizi, Profesa Bernadeta Killian alisema rais huyo alikulia katika familia iliyothamini elimu na alisoma masomo ya utawala wa umma, diplomasia na mahusiano ya kimataifa.
“Aliondoka nyumbani akiwa bado mdogo na kujiunga na harakati za ukombozi akiwa uhamishoni, akitumia ujana wake kupigania uhuru wa Namibia,” alisema Profesa Killian.



