JK: Samia atapata kura za kihistoria Pwani

PWANI : RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amesema mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan atapata kura za kihistoria Pwani kwa sababu anajali wananchi kwa kushughulikia changamoto zinazowasibu kwa haraka.
Kikwete alisema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara wa kunadi wagombea wa CCM uliofanyika Kibaha mkoani Pwani na kusisitiza kuwa mkoa huo haujawahi kuchanganya pumba na mchele kwa sababu wanajua madhara yake, hivyo Samia atashinda kwa kishindo kikubwa. SOMA: Mradi wa gesi Kinyerezi–Chalinze kujengwa
Aliongeza kuwa wananchi wa mkoa huo watamchagua Samia pamoja na wabunge na madiwani wa CCM kwa sababu mara zote amekuwa akizikabili changamoto za Watanzania kwa mafanikio makubwa.

Alisisitiza kuwa siku zote mcheza kwao hutunzwa hivyo ni wakati kwa wananchi wa Pwani kumtunza Samia kwa kura za kutosha kutokana na wema aliowatendea wananchi wa mkoa huo. “Mkoa wa Pwani unatambua umuhimu wa kukuwezesha kufanya kazi kwa mafanikio kwa kukupa kura za kutosha pamoja na kukupa wabunge na madiwani.
Hatuko tayari kuchanganya pumba na mchele kwa sababu tunajua madhara yake,” aliongeza Kikwete. Aidha, Kikwete alimwombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema na apate ushindi mkubwa ili aweze kuendelea kuliongoza taifa kwa weledi na ujasiri.
“Umeiongoza nchi yetu vizuri, wewe ni mama mwema unayejali changamoto zinazowasumbua wananchi unaowaongoza na pia ni mwepesi kuchukua hatua,” alisisitiza Kikwete Alisema tangu Samia aingie madarakani, Muungano umezidi kuwa imara zaidi na utaendelea kuwa imara.



