JKCI kuimarisha huduma tiba ya moyo nje ya Dar

DAR ES SALAAM; TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imepanga kuongeza huduma za matibabu ya moyo kwa maeneo nje ya Dar es Salaam.
Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam leo Julai 31, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge wakati akizungumzia kuhusu maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo Septemba mwaka 2015.
“JKCI inalenga kuongeza huduma za matibabu ya moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato, Lumumba Zanzibar na Arusha Lutheran (Seriani) Medical Centre kupitia program za uhamasishaji na uchunguzi wa moyo,” amesema Dk. Kisenge.

Ametaja mikakati mingine ya kupanua huduma zake ni ujenzi wa jengo la watoto wenye matatizo ya moyo katika eneo la Mloganzila na kwamba utaongeza uwezo wa taasisi kutoa huduma za moyo wa wagonjwa wengi zaidi.
“Taasisi inaendelea kuwekeza katika utafiti wa magonjwa ya moyo ili kuboresha mbinu za matibabu na kuzuia magonjwa haya,” amesema.



