Juhudi zinahitajika kutangaza vivutio vya asili vya mijini

TANZANIA imejaliwa vivutio vingi vya asili vilivyoko katika maeneo tofauti tofauti kwenye kila pembe ya taifa hili, kuanzia mijini hadi vijijini. Ni ukweli kuwa asilimia kubwa ya vivutio vya asili vinapatikana maeneo ya vijijini kuliko mijini lakini haina maana kuwa mijini hakuna vivutio vya asili.
Vipo vivutio vya kutengeneza na vikavutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi katika maeneo ya mijini lakini vipo pia vivutio vya asili ambavyo vinapatikana maeneo ya mijini. Kutokana na kutotangazwa vya kutosha, wananchi wengi katika maeneo ya mijini wamezoea kutembelea vivutio vya kutengeneza hali inayowafanya waamini kuwa katika maeneo ya mijini au karibu na miji hakuna hakuna vivutio vya asili.
Hili si kweli, kwa sababu mijini na maeneo yaliyopo jirani na mijini kuna vivutio vya asili na mfano mzuri ni Hifadhi ya Asili ya Pugu Kazimzumbwi iliyopo Kisarawe pembeni ya Jiji la Dar es Salaam. Hii ni hifadhi nzuri ya misitu ya asili ambayo ndani yake kunapatikana vivutio mbalimbali vitakavyomfanya mtalii kutojutia kuitembelea.
Hifadhi hii inahitaji kutangazwa zaidi kwa sababu imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, kutokana na kazi yake ya kufyonza hewa chafu inayozalishwa na pia kutoa hewa safi kulilisha jiji hilo. Ni dhahiri kuwa vivutio vilivyoko katika hifadhi hii vya asili, haviwezi kufananishwa kwa vyovyote na vivutio vilivyoko katika hifadhi za kutengeneza katika maeneo ya mijini na jirani na mijini.

Ndani ya Hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi kuna bwawa kubwa la maji linaloitwa Minaki lenye maji yanayotokana na chemichemi iliyopo ndani ya hifadhi, hali iliyopendezesha hifadhi na kuifanya muda wote kuwa ya kijani.
Moja ya raha za bwawa hilo ni upigaji wa makasia kwa watalii wote wanaotaka kufanya shughuli hiyo, huku uzuri wa maji yake ukileta raha inayochangiwa na baridi inayopatikana hata wakati wa jua la saa nane mchana. Pia, katika Hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi kuna vivutio vingi kama vile mapango mazuri ya mizimu na popo, miti ya mianzi ya miiba inayokua na kuongezeka usiku pekee na kambi nzuri za mapumziko.
Vivutio vingine ni pamoja na maeneo mazuri ya kufanya mazoezi ya kupanda milima, wanyama wazuri jamii ya mbega, ndege wanaohama kwenda na kurudi Ulaya pamoja na panzi Tanzania mwenye rangi za bendera ya taifa. SOMA: Samia avutiwa uhifadhi, ulinzi vivutio vya utalii

Tunaomba wadau wa masuala ya utalii, ikiwa ni pamoja na serikali kuhakikisha hifadhi kama hizi zinatangazwa vyema ili wananchi wajue, kwani wakati mwingine wanashindwa kutembelea vivutio vya asili kutokana na umbali lakini wakijua vivutio vilivyoko mijini watavitembelea.
Kwa kufanya hivyo, wananchi wanaoishi maeneo ya mijini watajua aina ya vivutio na umuhimu wa vivutio hivyo katika maisha yao. Kadhalika, watafanya uamuzi sahihi ya kuvitembelea kwa sababu vipo jirani hivyo hawatatumia gharama kubwa na pia vitawafanya kuwa mbali na changamoto za mijini na kupata ladha tofauti ya maisha na pia kuwakumbusha maisha ya kijijini.



