Kairuki aahidi kuimarisha barabara, maji na ajira Kibamba

DAR ES SALAAM: MGOMBEA Ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Kibamba, Angellah Kairuki, amesema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha barabara zote za jimbo hilo zinajengwa kwa lami na upatikanaji wa maji ni wa uhakika.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni mwishoni mwa wiki, Kairuki aliwahakikishia wananchi kuwa barabara kuu na za vijijini, ikiwemo Kibamba-Magohe-Mpiji, Lake Victoria-Magohe-Mpiji-Bunju na Mbezi-Victoria-Bunju, zitawekwa lami kwa awamu. Pia aliahidi kuboresha vivuko, makalvati na miundombinu ya barabara katika maeneo yenye changamoto, ikiwemo Mzulu, Goba, Ebonite, Ebeneza na Kingazi.
SOMA: Samia ataja kilimo, nishati, viwanda Iringa
Mgombea huyo alisema jimbo la Kibamba lina miradi zaidi ya 30 yenye thamani ya Sh bilioni 50.1 itakayotekelezwa. Kuhusu maji, alisema miundombinu ya Bangulo na Tegeta ina uwezo wa kuhifadhi lita milioni 16, na aliahidi kusimamia usambazaji, kuimarisha miundombinu na kuondoa ubambikaji wa bili.

Aidha, Kairuki alisema ataanzisha vituo vya ubunifu kwa vijana, kuimarisha viwanja vya michezo, kuendeleza mashindano ya Kairuki Cup, na kuanzisha kituo cha uwezeshaji wanawake. Aliahidi pia kuimarisha lishe mashuleni, kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya, kuendeleza mafunzo ya TEHAMA, na kufungua fursa za biashara na ajira kwa vijana na wanawake.
Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, John Mongella, aliwataka wanakibamba kuunga mkono kampeni hiyo na kuhakikisha Dk. Samia Suluhu Hassan anashinda kwa kura nyingi.



